Watumishi hao wakiongozwa na Diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri Mh Egnatio Mtawa wamempa pole Mama mlezi wa watoto hao Bi Bertina Mbilinyi na kusema msiba huo umewagusa wote
Wamesema wanatambua mchango wa mama huyo mlezi aliyeishi nao kwa miaka 7 tangu walipoanza darasa la kwanza mpaka darasa la 7 na ndiye aliyewafundisha mambo mengi na bado walikuwa wanamtambua kama mama yao mpaka walipofikwa na umauti
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya serikali Mwenyekiti wa Halmashauri Mh Egnatio Mtawa amesema serikali ngazi ya wilaya chini ya Mkuu wa wilaya Mh Veronica Kessy itashirikiana naye mwanzo mpaka mwisho wa msiba huo na kwa sasa inaandaa rambirambi kwa ajili ya kumkabidhi mama huyo mlezi
Kwa upande wake Mama mlezi wa Marehemu Maria na Consolata Bi Bertina Mbilinyi amewashukuru watumishi hao kwenda kumpa pole kwani amejisikia faraja japo msiba huo unampa machungu kwa jinsi alivyoishi na watoto hao muda mrefu
"Nilikwenda kuwatembelea wakiwa wamelazwa hospitali Dar es salaam na sikuwa na kitu cha kuwapa lakini nilipowauliza mnataka niwape nini walisema mama tunataka supu ya kuku" amesema mama huyo mlezi
Amesema kwa sasa anajiandaa kwenda Iringa kwa ajili ya maziko yanayotarajiwa kufanyika Tosamaganga jumatano ya wiki hii