Wanachama wapya 1457 Wajiunga na CCM

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein amewasisitiza Mabalozi kutowaunga mkono wale wote walioanza kutangaza nia ya kugombea nafasi za uongozi katika Majimbo kabla ya muda uliowekwa na chama hicho kufika na badala yake aliwataka waendelee kuyaimarisha Mashina yao ili kuipa ushindi CCM.

Dk. Shein ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo leo katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani mjini Unguja, wakati alipozungumza na Mabalozi wa Wilaya ya Amani Kichama.

Alieleza kuwa wapo baadhi ya wanachama wa chama hicho huanzisha makundi ya watu wachache na kujipanga katika kutafuta nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kabla ya muda kufika.

Aliongeza kuwa huo si mtindo mzuri na si utaratibu wa chama hicho na kueleza kuwa wanachotakiwa ni kusubiri wakati ukifika na wapo wanaovunjiana heshima wenyewe kwa wenyewe na kukivunjia heshima chama chao.

Makamu Mwenyekiti huyo aliwataka wanachama hao kusubiri wakati ukifika ndipo washindane na kuwataka kuachana na tabia hiyo ambayo sio nzuri na iwapo wataendelea na tabia hiyo hatua kali za kichama zitachukuliwa kwani tayari indhari imeshatolewa na viongozi wote wa ngazi za juu.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao kuyatangaza mafanikio ya Serikali na Chama chao yaliofikiwa katika maeneo yao.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kujitolea na kuwaeleza Mabalozi hao kuwa Zanzibar na hata Tanzania Bara zote zimejikomboa kwa njia ya kujitolea.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kueleza miradi mbali mbali ya maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa hapa Zanzibar na ambayo tayari imeshaanza kutekelezwa ukiwemo Mradi wa Mji wa Fumba huku akieleza azma ya Serikali kwa mashirikiano na wawekezaji kujenga Mji wa kisasa maeneo ya Chumbuni, Kwahani, Kisima majongoo na sehemu nyenginezo.

Aliwapongeza viongozi wa Wilaya na Mkoa wa CCM kwa kuingiza wanachama wapya 1457 na kueleza haja ya kuzisoma na kuzirejea ahadi zinazotolewa na wanachama wa chama hicho wakati wakila viapo vya kujiunga katika chama hicho ili waweze kukitumikia vyema chama chao.

Dk. Shein alitoa ahadi ya kumalizwa kwa ujenzi wa barabara ya Mboriborini huku akitoa shukurani kwa WanaCCM kwa kuwapigia kura nyingi viongozi wote wa chama hicho katika Makutano Mkuu wa CCM uliopita.

Miongoni mwa wanachama wapya waliojiunga na CCM na kukabidhiwa kadi na Makamo Mwenyekiti huyo ni pamoja na aliyekuwa mgombea wa Ubunge wa Chama Cha CUF mwaka 2015 Jimbo la Gando  Salim Mussa Omar.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo