Ikiwa ni siku moja imepita tangu shirikisho la soka nchini (TFF), liitumie barua Yanga ya kuitaka kuitisha uchaguzi wa kuziba nafasi zilizopo ikiwemo ya Mwenyekiti, mapya yameibuka yakimhusisha Ridhiwani Kikwete kuitaka nafasi hiyo
Baada ya tetesi hizo, Ridhiwani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze amesema hana lengo la kutaka uongozi ndani ya klabu hiyo kwa sababu yeye ni shabiki na hana kadi ya uanachama wa Yanga hivyo hana sifa za kugombea uongozi.
“Sina lengo lolote la kutaka uongozi ndani ya Yanga labda wanachama wenyewe ndio wanatengeneza maneno hayo lakini mimi binafsi hakuna sehemu nimewahi kutamka kwasababu hata sifa tu sina mana sina kadi ya uanachama,'' amesema.
Aidha Ridhiwani ameongeza kuwa mara kadhaa watu wa Yanga wamekuwa wakiomba ushauri juu ya nini cha kufanya na amekuwa akishauri kama shabiki wa kawaida na hajawahi kuwaambia kama anahitaji kuwa kiongozi.
Yanga imeitisha mkutano mkuu wa wanachama mwezi ujao na huenda agenda kubwa ikawa ni uchaguzi kuziba nafasi ya Mwenyekiti ambayo ilikuwa inashikiliwa na Yusuf Manji kabla ya kujiuzulu mwaka jana.