Watuhumiwa wa Mauaji wakutwa na Orodha ya "Kill Them All"

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu watano akiwemo mganga wa kienyeji kwa tuhuma ya kujihusisha na mauaji ya kukata mapanga wanawake katika kata ya Salawe Shinyanga vijijini kutokana na imani za kishirikina.
 
Hayo yamebainishwa leo Aprili 6,2018 na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo kwenye mikutano ya hadhara miwili iliyofanyika katika kijiji cha Mwenge na Songambele. 

Amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuhusika na mauaji hayo kuwa ni Stephano Maduka (20), Nihinga Lendele (57) Reuben Mafura (30) Amosi Itawa (21) pamoja na mganga wa kienyeji Itawa Ming’hwa (47) ambapo wote wapo chini ya ulinzi wa jeshi hilo na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili. 

Amesema walipofanya upekuzi nyumbani kwa mganga huyo wa kienyeji alikutwa akiwa na mkia wa mnyama adhaniwaye kuwa ni nyati, ngozi ya kenge, kipande cha ngozi ya Fisi, Pembe nne za wanyama mbalimbali,shuka tano nyeusi za kaniki, karatasi nakala tatu zenye maandishi “KILL THEM ALL” kifaranga cha kuku kinachotumika kupigia ramli chonganishi. 

Ametaja vitu vingine kuwa ni chupi moja ya kike, mafungu mbalimbali ya mchanga, mawe yadhaniwayo kuwa ni madini ambayo yanatumika kupigia ramli chonganishi, pamoja na karatasi ikiwa na majina ya wanawake tisa ambao wamepangwa kuuawa ili kukamilisha ushirikina huo. 

“Baada ya kuwahoji watuhumiwa hao baadhi yao wamekiri kuhusika na mauaji haya kwa madai waliagizwa na waganga wa kienyeji kwa kutoa kafara za wanawake tisa kama ndagu ili dawa zipate kufanya kazi na kupata utajiri,”,amesema Haule 

Pia Kamanda  Haule amewataja wanawake watatu ambao wameshauawa kwenye imani hizo za kishirikina kuwa ni Mwalu Misri (24) Salome Paschal (24) Kabunga Linonelwa(10) ambao waliuawa kwa nyakati tofauti kuanzia kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu kwa kuviziwa kwenye vichaka na kisha kuuawa. 

Katika hatua nyingine Kamanda ametoa wito kwa wananchi hasa vijana kuacha kutafuta mali kwa njia za ushirikina bali wajiunge kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze kukopesheka na kufanya kazi halali ambazo zitawaingizia kipato na kuinuka kiuchumi. 

Nao baadhi ya wanawake waliohushuria kwenye mikutano hiyo ya hadhara Neema Paulo na Happynes Jeremia wameiomba serikali kukomesha kabisa matukio hayo ya mauaji dhidi yao ambayo yamekuwa yakiwafanya kushindwa kwenda kufanya shughuli za kiuchumi ikiwamo mashambani kwa kuhofia kuuawa. 

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo