
Tukio hilo lililodumu kwa takribani dakika 45 limetokea leo Jumamosi Aprili 7,2018 saa tano asubuhi.
Mwanaume huyo anayekadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 40 alikuwa amevaa nguo nyekundu,kofia nyekundu yenye msalaba,biblia,mito,midoli,msumeno,baiskeli na majembe yenye mipini ya nondo.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa jamaa huyo alifika katika eneo la Ushirika karibu na ofisi za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kisha kusimama kwenye eneo la kuvukia ‘Zebra’ akaanza kusimamisha magari.
“Alifika hapa akiwa amevaa joho jekundu kama la kiaskofu pamoja na kofia nyekundu yenye msalaba huku akiwa ameshikilia biblia,baiskeli,msumeno na majembe,akatandaza barabarani vitu alivyokuwa navyo akawa anasimamisha magari huku akisema yeye ni Malkia wa Nguvu ametumwa na Mungu kuja Kukomboa nchi ya Tanzania”,wameeleza mashuhuda wa tukio hilo.
Aidha wamesema wakati akisimamisha magari alisikika akisema bado usiku ,hapajakucha wasiendelee na safari na kwamba yeye ametumwa kuja kukomboa nchi.
“Alisimamisha kila gari pande zote mbili,akasababisha foleni ndefu,dereva wa basi la Mgamba lililokuwa linatoka Mwanza alipogoma kusimama ndipo jamaa akapasua kioo cha mbele akitumia majembe yake ambayo yamechomelewa nondo”,waliongeza mashuhuda.
Kufuatia taharuki hiyo jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na kumkamata mwanaume huyo ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi wowote akisema wampeleke tu kwenye vyombo vya sheria kwani yeye hana kosa bali amekuja kukomboa nchi.
Hata hivyo inaelezwa kuwa jana jamaa huyo ambaye hajulikani ametokea wapi alionekana eneo la Ushirika akiwa amevaa kanzu nyeupe na kofia 'kibaraghashia' na hata juzi alifika katika ofisi za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga zilizopo hapo Ushirika.
na Kadama Malunde
Mwanaume huyo akipelekwa kwenye gari la polisi
Askari polisi wakimpeleka jamaa huyo kwenye gari la polisi
Mwanaume huyo akipelekwa kwenye gari la polisi
Jamaa akipanda kwenye gari la polisi
Askari polisi akiwa ameshikilia msumeno na majembe mawili ya mwanaume huyo