Lile sakata la Mkurugenzi wa Kampuni ya CZI, ndugu Cyprian Musiba, kuwahusisha baadhi ya makada wa CHADEMA katika orodha yake ya kile alichokiita kama watu hatari kwa usalama wa Tanzania, limezua sura mpya baada ya uongozi wa CHADEMA kuziandikia barua balozi za Marekani na Ujerumani kuhusu tuhuma hizo ambapo ndugu Musiba alizitaja nchi hizo kushirikiana na baadhi ya watu katika orodha yake kuhatarisha usalama wa taifa.
Kwa mujibu wa habari iliyochapishwa na gazeti la Mtanzania la Machi 3, 2018, imedai kuwa CHADEMA iliandika barua hizo Machi 1, 2018 na kusainiwa na mkuu wa kitengo cha habari wa chama hicho, Tumaini Makene, ikizitaka balozi hizo nchini kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwa nchi hizo na ndugu Musiba.
Habari zinasema katika barua yenye kumbukumbu No. C/HQ/ADM/KS/24/02 ambayo imeelekezwa kwa John Espinos ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi, Ubalozi wa Marekani, Chadema imeeleza kwamba Februari 25, mwaka huu mtu aliyejulikana kwa jina la Cyprian Musiba, aliituhumu Marekani kwa kufanya mipango na mikakati mbalimbali ya kuhatarisha usalama wa Taifa la Tanzania.
Aidha habari zinasema kuwa CHADEMA iliandika barua ya pili yenye kumbukumbu No. C/HQ/ADM/KS/24/01 ambayo ilielekezwa kwenda kwa Joerg Hererra ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi cha Ubalozi wa Ujerumani, Chadema ilisema Musiba alikaririwa akikituhumu chama tawala cha nchi hiyo cha Christian Democratic Union (CDU) kushiriki mipango ya kuhatarisha usalama wa Tanzania.
Jumapili iliyopita ndugu Cyprian Musiba ambaye alijitambulisha kama Mkurugenzi wa Kampuni ya CZI, alimtuhumu mtanzania aishiye nchini Marekani, Mange Kimambi, kushirikiana na kitengo cha FBI (Federal Bureau of Investgation) kupanga machafuko hapa nchini.
Musiba pia alikituhumu chama tawala cha Ujerumani kiitwacho Christian Democratic Union (CDU) kushirikiana na wanasiasa wa upinzani katika mipango mbalimbali inayohatarisha usalama wa taifa la Tanzania.
Orodha ya watu hatari kwa usalama wa taifa iliyotolewa na ndugu Musiba inawajumuisha: Mange Kimambi, Freeman Mbowe, Maria Sarungi, Zitto Kabwe, Tundu Lissu, John Heche, John Marwa, Evarist Chahari, Julius Mtatiro, na kikundi cha Janja Weed alichodai kinaratibiwa na wafuasi wa CUF.
