Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Mwigulu Nchemba amevunja ukimya kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania-TSNP, Abdul Nondo aliyemtaka ajiuzulu kwa madai kuwa ameshindwa kutekeleza jukumu lake la kulinda usalama wa raia kufuatia uwepo wa matukio ya baadhi ya watu kupotea na wengine kuuliwa na watu wasiojulikana.
Dkt. Nchemba wakati anazungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-UDSM leo, amesema tangu Nondo atoe kauli hiyo hakujua kama ilimlenga yeye na badala yake alijua ilimlenga pengine Waziri wa Srikali ya wanafunzi wa chuo hicho- DARUSO au waziri mwengine.
“Rafiki yangu nilitaka nimuone sana hapa Nondo, eti anasema waziri ajiuzulu halafu amekaa mpaka muda fulani mimi hata sikujua kama anasema waziri wa mambo ya ndani, mimi nilifikiri waziri wa daruso ama wapi kule,” amesema.
“Ukiona mwanazuoni ana lalamika kama Rema ujue kuna kasoro, kama sasa hivi tuna masuala ya muhimu ya serikali ambayo mtanzania yoyote bila kujali chama chake unatakiwa usimame na rais kwa hatua alizochukua, siku ya kampeni ni kitu kingine lakini vitu ambavyo rais anafanya ni urithi wa watanzania wa sasa na baadae kuwa mwema katika vyuo vikuu siyo kuwa kimya.”
