WAJUMBE wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nachingwea, mkoa wa Lindi, wakataa kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho iliyoandaliwa na mkuu wa idara ya ushirika ya halmashauri ya wilaya hiyo.

Hayo yalijiri wakati wakikao kilichofanyika katika ukumbi wa chuo cha walimu kilichopo katika mamlaka ya mji mdogo wa Nachingwea. Wakizungumza kwenye kikao hicho kilichokuwa na lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya 2015 – 2020 kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2017, wajumbe hao walisema taarifa ya mkuu huyo wa idara ya ushirika haikujibu mahitaji ya msingi na haikuandaliwa vizuri. Hivyo hakukuwa nahaja ya kuendelea kujadili kabla ya kufanyiwa marekebisho.
Wajumbe hao walikwenda mbali kwakusema mkuu huyo wa idara anaweza kuwa nimiongoni mwasababu zitakazo sababisha wananchi, hasa wakulima wa korosho wakichukie chama hicho na serikali yake. George Kasembe, ambae pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Lindi, alisema iwapo mkuu huyo wa idara akiendelea kubaki katika wilaya hiyo atasababisha chama cha Mapinduzi (CCM) kichukiwe. Hasa wakulima wa korosho ambao kila mwaka wacheleweshewa malipo bila sababu za msingi.
Mjumbe huyo alisema miongoni mwa kasoro za utendaji za mtumishi huyo wa umma ni tabia ya kutegemea taarifa za kupelekewa ofisini kwake, badala ya kutembelea vyama vya msingi vya ushirika ili kuona hali halisi. “Hatembei kwenye vyama, anategemea taarifa za wahasibu wa vyama, gari anayo lakini hatembelei vyama. Huyu akiendelea kubaki ataharibu chama chetu,” alisisitiza na kuonya Kasembe.
Kauli ya Kasembe iliungwa mkono pia na mbunge wa jimbo la Nachingwea, Hassan Masala aliyetoa wito kwa wajumbe wenzake waachane na mkuu huyo wa idara. kwamadai kwamba anatakiwa kusaidiwa baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Huku akionya kwamba kuwapuuza ni kuharibu chama. Kwani katika wilaya hiyo siasa imeshikwa na kilimo. Kwahiyo kilimo ndio siasa yenyewe.
“Mkuu wa wilaya, kuendelea kusikia watendaji wamekamatwa wapo polisi hakutafanya wakulima walipwe. Nikuombe pia uliza huko polisi kwanini mambo yanaishia kwao badala ya mahakamani. Watendaji na viongozi wangapi wa vyama vya msingi wamefikishwa mahakamani. Tuchukue kuwa nitatizo na tulitafutie utatuzi badala ya kutegemea mtu anaetuambia na kutegemea polisi,” alionya na kushauri Masala.
Mbunge huyo pia alisema mkuu huyo wa idara amekuwa hasemi kweli. Akitoa mfano kwakusema aliwahi kumsikia kuwa ni vyama vitatu pekee havijamaliza kuwalipa wakulima wa korosho. Hata Hivyo katika kikao hicho alivitaja vyama zaidi ya sita.
Maelezo ya Kasembe na Masala yaliongezewa na katibu wa kata ya Nangowe, Ramadhan Mmoro, ambae alishauri taarifa ya mkuu huyo wa idara isiendelee kujadiliwa kabla ya kufanyiwa marekebisho. Ushauri ambao uliafikiwa na wajumbe wa kikao hicho. Kwa upande wake mkuu huyo wa idara, Lameck Chotta licha ya kupinga maelezo aliwaomba wajumbe hao watambue hakuna chuo kinachotoa mafunzo wala kozi ya uaminifu. Kwani miongoni mwa sababu za baadhi ya wakulima kuchelewa kulipwa ni wizi uliofanywa na makaraani na viongozi wa baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), ambao wamefikishwa kituo cha polisi.
Huku akibainisha kwamba wengine wameshalipa fedha walizokwapua. Mkuu huyo wa idara alitaja sababu nyingine ni baadhi ya wakulima kutofungua akaunti. Badala yake wanatumia za wenzao ambao huwaambia bado hawajalipwa, hata kama tayari wamelipwa. “Wahasibu, makaraani na wajumbe wa bodi walipata mafunzo, lakini baadhi yao ni hao wanaotenda kinyume. Hakuna mafunzo ya uaminifu, kwakuwa ni wezi tunawafikisha polisi hatuna njia nyingine. Sasa kutofikisha au kuwafikisha mahakamani sio jukumu langu,” Chotta alijitetea kwa kueleza baadhi ya sababu kuwepo wakulima wa korosho wasio lipwa hadi sasa.
Kwamujibu wa mkuu huyo wa idara ya ushirika takribani shilingi Bilioni 84.95 zilitokana na mauzo ya kilo 216, 641,426 za korosho wamelipwa wakulima wa zao hilo waliopo wilayani humu. Ambapo shilingi takribani milioni 109 tu ndizo zinazodaiwa na wakulima hao.