Waziri Majaliwa ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11 na kuahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.
"Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa watendaji wa elimu kuanzia Wakurungezi wa Halmashauri pamoja na wadau wote wa elimu kuzingatia maelekezo ya Waraka uliotolewa na Serikali, ambapo majukumu ya kila mdau katika kutekeleza Mpango wa elimu msingi bila malipo yamefafanuliwa", amesema Majaliwa.
Akizungumzia fedha zilizotolewa katika utekelezaji wa mpango huo, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2017, serikali imetuma moja kwa moja shuleni jumla ya sh. bilioni 124.8.
"Fedha zinazopelekwa moja kwa moja shuleni kwa mwezi ni shilingi bilioni 20.8 na shilingi bilioni 3.06 hupelekwa Baraza la Mitihani kwa ajili ya fidia ya gharama za mitihani kwa wanafunzi wa shule za serikali", amesema Majaliwa.
Pamoja na hayo, Waziri Majaliwa ameendelea kwa kusema "ruhusa ya michango shuleni ipo, kutoka mtu mmoja mmoja, vikundi au taasisi. Hata hivyo, michango yote sasa itafikishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili ashirikishe Kamati ya shule za msingi na bodi kwa shule za sekondari. Walimu wasisumbuliwe na michango ili wajikite na taaluma."
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu amesema serikali inaendelea kukusanya taarifa kutoka shule mbalimbali za sekondari za serikali kwa lengo la kujua hali ya umiliki wa ardhi katika shule hizo.