ROMBO: Kijana apewa pombe kali kisha kulawitiwa na wanaume wawili


Kijana wa miaka 20 amelawitiwa na wanaume wawili kwa wakati mmoja baada ya kusadikiwa kunyweshwa pombe kali katika kitongoji cha Kitefure, kijiji cha Lesoroma,Tarafa ya Usseri wilayani Rombo.

Kijana huyo alitoweka nyumbani kwao siku ya Jumamosi baada ya kuchukuliwa na watu hao ndipo baadaye alifanyiwa ukatili huo bila ya yeye kufahamu.

Akizungumza na gazeti hili leo Februari 9 kijana huyo amesema kuwa watu hao walikuja nyumbani kwao huku wakitaka kwenda kwenye klabu ya pombe na ndipo baadaye alijikuta yuko kichakani huku akiwa na maumivu makali. 

"Sijui niliwakosea nini kwenye pombe ambayo nilikua nakunywa, sijui waliniwekea kitu gani, hapa nilipo napata maumivu makali sana," alisema kijana huyo.

Baada ya hali ya kijana huyo kuwa mbaya akiwa Hospitali ya Huruma iliyoko Rombo, alihamishiwa hospitali ya Mkoa, Mawenzi kwa matibabu zaidi.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lesoroma,Emma Mosha amesema kuwa kijiji hicho kimekuwa na vitendo vingi vya ukatili kutokana na kushamiri kwa pombe haramu ambazo zimekua kero kwa baadhi ya familia. 

Amesema baada ya kupata taarifa hizo ameshirikiana na familia ya kijana huyo ili waliohusika kufanya kitendo hicho wakamatwe.

"Kwa kweli kitendo alichofanyiwa kijana huyu ni kibaya sana na cha aibu, tutashirikiana pamoja ili waliofanya kitendo hiki kiovu wakamatwe," amesema mtendaji

Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Kilimanjaro, Koka Moita aliwataja watu wawili kuwa ndio wanaotuhumiwa kufanya ukatili huo ambao wote ni wakazi wa Kitefure, kijiji cha Lesoroma.

Kamanda Moita amesema kuwa Jeshi la polisi linafanya msako wa kuwakamata watuhumiwa hao 

"Hawa watu wamechelewa kutoa taarifa mapema ndio maana hawa watuhumiwa wametoroka lakini tutahakikisha wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo husika," amesema Kamanda.

Chanzo: Mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo