WAHUDUMU wa mochari katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) wameandamana kupinga madai ya kuhusishwa na ubakaji wa kina mama katika hospitali hiyo.
Wakibeba mabango yaliyokuwa na jumbe tofauti, wahudumu hao waliokuwa ni pamoja na wafanyikazi wengine wa hospitali hiyo walikana madai hayo, kwa kusema wao si wabakaji.
“Sisi ni wananchi wa Kenya na tunastahili heshima na pia tunafaa kulindwa. Sisi sio wauaji, sisi ni wataalamu wanaowajibikia taifa na watu wake,” amesema mmoja wa waandamanaji hao.
Wameshangaa sababu ya kuibuliwa kwa madai hayo wiki jana licha ya kuwa kwa miaka na mikaka wamekuwa wakifanya kazi KNH ila hakujawahi kuwa na malalamishi yoyote.
Wamesema wao hawakuwa wanasiasa na kuongeza kuwa wao hufanya kazi kwa bidii.
Wameonekana kutetea hospitali hiyo iliyo kubwa zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na ambayo hutibu wagonjwa hasa kesi za rufaa.
“Hii sio taasisi ya kisiasa, hii ni taasisi ya afya, sio uwanja wa siasa, mkitaka siasa zimo Bungeni. Achaneni na wagonjwa wetu, wahudumu wetu na madaktari wetu,” amesema mhudumu huyo.
Kumekuwa na maandamano mengi kuhusiana na madai kwamba kina mama katika hospitali hiyo walikuwa wakibakwa wakielekea kunyonyesha watoto wao katika wadi iliyo orofa ya kwanza ndani ya hospitali hiyo.
Kujiuzulu
Kundi la wanawake limeandamana hadi Jumba la Afya na kumtaka Waziri wa Afya Dkt Cleopa Mailu kujiuzulu.
Kundi hilo lilikuwa limefika katika jumba hilo kuwasilisha ombi kwa waziri huyo kumaliza mgogoro unaoendelea KNH, licha ya kumtaka kujiuzulu.
Jumatatu, kundi lingine la wanaharakati liliandamana kutokana na madai hayo.
Jumamosi, viongozi wa kike walizuru hospitalini humo na kufanya ziara ili kukusanya habari kuhusiana na suala hilo.
Walipendekezea hospitali hiyo kuwahamishia kina mama karibu na watoto wao ili kuepuka visa kama hivyo ikiwa madai hayo yalikuwa ya kweli.
Bodi ya hospitali hiyo tayari imeidhinisha kuhamishwa kwa kina mama karibu na watoto wao, huku uchunguzi wa madai hayo ukiendelea. Tayari, KNH imekana kupokea ripoti zozote kuhusu ubakaji.
