Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Shaidi Mchembe ameagiza kukamatwa kwa viongozi wote waliofuja shilingi milioni 32 za ujenzi wa shule ya sekondari ya Kata ya Idibo.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati alipofanya ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo lililokwenda sambamba na ugawaji wa mabati na vifaa mbali mbali kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Idibo.Mhe. Mchembe aliwaomba TAKUKURU kuwakamata viongozi wote wanaosimamia ujenzi wa shule ili waweze kuhojiwa matumizi ya pesa na wizi uliotokea tokea kuanza kwa ujenzi huo.
"Nimepokea taarifa ya Kamati ya Ujenzi ambayo imebaini wizi wa shilingi milioni 12 na matumizi ya utata yenye thamani ya shilingi milioni 20, hivyo ninawaagiza TAKUKURU na OCD ndani ya siku saba kuwakamata wale wote wanaohusika na sheria ichukue mkondo wake," alisema Mhe. Mchembe.
Aidha mpaka sasa japo kuna dosari Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata Idibo umemaliza madarasa 3, vyoo na jengo la utawala.Wakati huo huo Mhe. Mchembe alikabidhi msaada wa mabati 120 na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kupanua kituo cha Polisi Idibo kilichojengwa kwa nguvu za wananchi.
Katika hafla hiyo, Mhe. Mchembe aliyepokelewa na mwenyeji wake OCD - Gairo, Mratibu Mwandamizi Jeshi la Polisi, Ramadhani Kitantu, alitoa pongezi kwa Diwani Kata ya Idibo Mhe. Rajabu Mguhi na viongozi wake wote na wananchi wa Idibo kwa michango yao hadi boma kukamilika.
Mhe. Mchenbe aliwaomba wananchi washiriki kuchangia awamu ya pili ya umaliziaji bila kusahau nyumba za Polisi. Pia anakaribisha Wadau wengine wa maendeleo wenye Mapenzi mema na Gairo TUSHIRIKIANE.
Katibu Tawala Wilaya Bw. Adam John wakati wa ziara hizo alisisitiza wananchi kushirikiana na Serikali ili kujiletea Maendeleo yao. Pale ambapo kuna matatizo atahakikisha anayashughulikia ipasavyo kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni (STK). Ndani ya mwaka mmoja tumefanikiwa kufungua Sekondari za Kata mbili ambazo ni Chagongwe na Chanjale. Kote huko watoto walikuwa wanatembea zaidi ya km 20 kwenda shule na maabara sita.
Miradi yote ni nguvu za wananchi kwa zaidi ya asilimia 45 na fedha kutoka Serikali. Pongezi kwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali watoto wa masikini huku pembezoni vijijini kabisa ambapo nao wanajisikia vizuri na wanajenga Uzalendo wa kuipenda nchi yao tangu wadogo.
Gairo ina kituo kimoja tu cha Polisi hivyo hiki kitakuwa cha pili. Kituo hiki kitahudumia Kata tano za Gairo na Kata jirani zaidi ya sita kutoka Wilaya ya Kilindi, Kiteto na Mvomero kwani kipo mpakani mwa Wilaya hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Shaidi Mchembe (kushoto) akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita na OCD - Gairo, Mratibu Mwandamizi Jeshi la Polisi, Ramadhani Kitantu (kulia) wakati alipofanya ukaguzi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Idibo, shule ya sekondari ya kata ya Idibo sambamba na ugawaji wa mabati na vifaa mbali mbali kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Idibo.