Wafanya sherehe kufurahia kuuawa Fisi 15

Mamia ya wakazi wa kijiji cha Buzanaki kata ya Nyamarimbe katika mkoa wa Geita, wamesherehekea kuuawa kwa fisi 15 hadi jana, katika matukio tofauti wiki moja baada ya mtoto wa miaka sita kuliwa na wanyama hao na wengine watatu kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Yusufu, Martha Musa na Simon Balele walidai marehemu alikamatwa na fisi saa moja jioni Desemba akiwa na watoto wengine wanne ambao baada ya tukio walikimbia na kutoa taarifa.

Desemba 2 mabaki ya mwili wa mtoto Yusufu yalipatikana kijijini hapo yakiwa yamebakia utumbo na mfupa mmoja wa paja ambavyo ndivyo vilivyozikwa kwa heshima ya familia.

Kutokana na tukio hilo, wanakijiji chini ya Mwenyekiti wa Kijiji Robert Maholosha, Ofisa Mtendaji, Rose Paul walitangaza msako wa fisi ulioongozwa na kuratibiwa na Musese Kabulizina ambaye ni ofisa wanyamapori wilaya ya Geita.

Hadi jana fisi 15 walikuwa wameuawa katika matukio tofauti katika kijiji cha Buzanaki fisi 6 na katika kijiji cha Idoselo fisi 9 wameuawa ambako nako wanakijiji watatu walijeruhiwa.

Kwa mujibu wa ofisi ya wanyamapori wilaya ya Geita mwaka 2010 hadi 2014 watu saba waliuawa na fisi huku mwaka 2017 ameuawa mtoto mmoja na wengine watatu kujeruhiwa.

Hata hivyo, tukio la Mei 7 mwaka 2012 lililotokea katika kijiji cha Luezera ndilo lililotisha zaidi kwani baada ya fisi kumkamata mtoto mwenye umri wa miaka 8 saa moja jioni wakati akitoka dukani kununua mafuta ya taa na kutoweka naye kuliibuka sintofahamu kubwa.

Katika tukio hilo, wanakijiji kadhaa walihamasishanana kuwaua watu watatu kwa marungu, mapanga na fimbo wakiwatuhumukuwafuga fisi hao kwa ajili ya ushirikina.

Katika tukio hilo pia wanakijiji hao waliteketeza nyumba 5 za familia tofauti kwa moto huku mzee mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 akijinyonga kwa kuhofia naye kuuawa kwa kipigo na wananchi baada ya kutuhumiwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa.

Hata hivyo, Musese Kabulizina, Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ameionya jamii kutoyahusisha matukio ya fisi na imani za kishirikina na badala yake anasema kuwapo kwa fisi wengi katika makazi ya watu ni matokeo ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa wanyamapori wakiwamo fisi kuanza kuvamia makazi ya binadamu kusaka mahitaji kikiwamo chakula.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo