Shahidi aeleza sababu za kumtolea Lema bastola

Moses Mashalla,Mwananchi 
Arusha. Shahidi wa kwanza katika kesi ya kudaiwa kumdhalilisha Rais John Magufuli inayomkabili Mbunge wa jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema ameieleza mahakama kwamba  alimtolea bastola mbunge huyo  kwa sababu alikuwa akijaribu kutoroka.
Shahidi huyo, Damas Masawe (44) ambaye ni mkuu wa upelelezi wilaya ya Arusha(OC-CID)  ameileza mahakama hiyo kwamba mnamo Juni 22 mwaka jana alilazimika kuichomoa bastola yake katika eneo la kambi ya Fisi ambapo kulikuwa na mkutano wa hadhara uliokuwa ukihutubiwa na mbunge huyo.
Akitoa utetezi wake leo mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Sekei, Devotha Msofe shahidi huyo alisema sio kweli kwamba ana ugomvi na Lema kwa kuwa hata watoto wa mbunge huyo wanampenda sana.
Akijibu swali lililoulizwa na wakili wa upande wa utetezi, Sheck Mfinanga kwamba gari lake liliwahi kuchomwa moto na wafuasi wa Chadema mkoani Iringa katika mkutano ambao Lema alikuwa akihutubia shahidi huyo alikiri ni kweli gari lake lilichomwa moto lakini hawakuwa wafuasi wa Chadema.
Shahidi huyo aliiambia mahakama hiyo kwamba ingawa yeye sio mtaalamu wa masuala ya imani lakini anaamini kuota ndoto sio kosa lakini kosa ni kuhadithia ndoto .
Massawe ameiambia  mahakama hiyo kwamba maneno aliyoyatamka mbunge huyo laiti angeyatamka wakiwa  katika vikao vya nyumbani mkoani Kilimanjaro asingekuwa na shida lakini aliyatolea kwenye mkutano wa hadhara.
“Kuota ndoto sio kosa lakini kuhadithia ndoto yako ni kosa hayo maneno laiti ningekutana naye uchagani kama kaka yake angeniambia wala nisingekuwa na shida lakini aliyatolea mkutanoni” ameiambia mahakama
Hata hivyo, shahidi huyo amesema kwamba kwa mujibu wa kitabu cha biblia anachokijua yeye kinasema kwamba wazee pekee ndio wataota ndoto na wala sio vijana na hivyo Lema hakustahili kuota ndoto dhidi ya Rais Magufuli kwa kuwa bado ni kijana.
Shahidi huyo amesema  kwamba Lema hajafikisha umri wa miaka 60 na hivyo hatakiwi kuota ndoto bali wazee ndio wanatakiwa wapumzike ,watafakari na kuota ndoto.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali, Agnes Hyera ulimtaka shahidi huyo kuieleza mahakama hiyo kwamba kulikuwa na idadi ya watu wangapi katika mkutano ambao Lema alitamka maneno hayo na kusema ni takribani watu 200.
Amesema  kwamba kitendo cha Lema kumwita Rais Magufuli ana kiburi na kumtabiria kifo ni kuamsha chuki kwa wananchi waliomchagua na hakupendezwa na maneno hayo na hivyo aliamua kumchukulia hatua yeye wakati akikaimu nafasi ya mkuu wa polisi wilaya ya Arusha.(OCD).
Kesi hiyo nambari inataraji 440 ya mwaka 2016 inataraji kuendelea tena mnamo Januari 22,23 na 24 ambapo upande wa mashtaka unataraji kuwaleta mashahidi wengine mbele ya mahakama hiyo.
Katika kesi hiyo  Lema anadaiwa kutoa maneno ya kumdhalilisha Rais Magufuli katika eneo la Kambi ya Fisi ambapo alitamka ya kwamba Rais Magufuli asipoacha kiburi chake cha kuminya demokrasia atakufa kabla ya mwaka 2020 .


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo