Tundu Lissu anadai kuwa kauli hiyo haina ukweli hata kidogo kwani kitendo cha yeye kusafirishwa kwa ndege mnamo Septemba 7, 2017 majira ya usiku kuelekea kwa matibabu nchini Kenya ni wazi kuwa kibali kilitolewa na serikali pamoja na Bunge kwani bila hivyo yeye asingeweza kusafirishwa.
"Mimi sikuamua kuja Nairobi sikuwa najitambua, watu walioamua mimi kuja Nairobi ni pamoja na Spika Ndugai mwenyewe watu wameniambia kwenye hicho kikao cha nipelekwe wapi Ndugai alikuwepo, Naibu wake alikuwepo, Katibu wa Bunge wakati huo Kashilila alikuwepo, Mwenyekiti wa chama changu alikuwepo ile ndege iliondoka saa sita usiku sasa ingerukaje kama haikuruhusiwa na serikali ya Tanzania kuruka kuja Nairobi? Kwa hiyo hii habari ya kwamba amepelekwa wapi ni mambo ya kujishikiza shikiza tu ni Bunge kujaribu kukwepa wajibu wake wa kisheria" alisema Tundu Lissu
Aidhaa Tundu Lissu aliendelea kufafanua kuwa "Nimesema mimi siombi fadhila, hakuna mtu anaomba kufadhiliwa hapa mimi naomba haki ambayo anatendewa mtu aliye Mbunge anayeumwa ambaye amelazwa nje ya kituo chake cha kazi hicho tu.
Mbali na hilo Tundu Lissu amesikitishwa na upelelezi unaofanywa na jeshi la polisi kuhusu shambulio lake la kutaka kuuawa na kusema anashangaa mpaka leo jeshi la polisi halijasema linamshuku nani kuhusika na shambulio hilo na mpaka leo jeshi la polisi halijaweza kumhoji japo aweze kutoa maelezo yake.
Tundu Lissu alishambuliwa na risasi mnamo Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma na baadaye kupelekwa nchini Kenya jijini Nairobi kupatiwa matibabu ambapo mpaka sasa yupo huko kwa matibabu.