Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mchungaji Peter Msigwa amefunguka na kuwataja wabunge watano wa chama hicho ambao wamepangwa kushughulikiwa na kuhakikisha hawarudi Bungeni 2020.
Msigwa amesema hayo alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari na kusema kuwa wapo watu kutoka serikalini na chama tawala wamekuwa wakimpigia simu na kutaka kumpa fedha ili aweze kujiuzulu nafasi yake hiyo ya Ubunge na kudai watu hao wamemweleza kuwa wabunge wa CHADEMA akiwepo yeye, Joseph Mbilinyi (Sugu), Halima Mdee pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema mwaka 2020 hawawezi kurudi tena bungeni.
"CHADEMA kipo imara na hakijayumba hata kidogo na hiki kinachoitwa wimbo la watu kuhama hama, kwa kifupi kuna baadhi ya simu na mimi nimezipokea baadhi ya watu wanajaribu kunitishia na kuniambia kwamba Msigwa ni bora tukupe hela kwa sababu mwaka 2020 wewe, Godbless Lema, Halima Mdee, Mnyika na Sugu hata mfanyaje mtaondoka kwa hiyo ni bora tu uchukue hela ili uhamie CCM" alisema Msigwa
Aidha Msigwa aliweka msimamo wake kuwa hata wafanyeje hawezi kuhama CHADEMA na kwenda CCM na kuwataka watu ambao wanampigia simu hizo waache kufanya hivyo, kwani yeye hanunuliki na wala hana bei.