Mahakama ya Vileo Zanzibar imeziruhusu baa zote 12 zinazofanya biashara ya Pombe Wilaya ya kati kuendelea na biashara hiyo kutokana na kukidhi vigezo na masharti ya kisheria yaliyowekwa na serikali.
Akitoa ruhusa hiyo huko katika Mahakama ya Wilaya Chwaka Mwenyekiti wa Mahakama hiyo Mohammed Subeit amesema Bodi ya ukaguzi imefanya ukaguzi katika baa zote zilizopo wilaya ya kati ikiwemo Chwaka, Uroa na Marumbi na imejiridhisha na utendaji wa wenye mabaa.
Amesema vigezo wanavyoviangalia katika ukaguzi wa baa nchini ni mazingira ya eneo la biashara, ukataji wa lessen na vibali kwa mmiliki wa biashara hiyo,kama eneo litakuwa na fujo au malalamiko ya wananchi sheria ya vileo inaruhusu baa hiyo kufungiwa lakini kama vitakuwa hakuna tatizo lolote hakutakuwa na pingamizi kwa mmiliki kunyimwa kibali cha kufanyia biashara.
Hata hivyo amesema wakati mahakama inaendelea na zoezi la kupokea maombi kwa wamiliki wa baa Watendaji wa mahakama hiyo hawakupokea malalamiko wala tuhuma zozote kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya kati kama baa hizo zinaleta usumbufu au matatizo yoyote.
Aidha Subeit ametoa wito kwa wamiliki wa baa kufuata sheria zilizowekwa na mahakama ya vileo na pindipo wataepuka kufuata maagizo waliyoambiwa mahakama haita sita kuzifungia baa au kuwapokonya vibali vya biashara hiyo.
Jumla ya baa 21 zimeruhusiwa kuendelea kufanya biashara ya pombe kwa mwaka 2018 kutokana na kukidhi vigezo.
Amina Omar Zanzibar24.