Eneo alilokutwa amezikwa marehemu
Katika hali isiyokuwa ya kawaida
Kijana Nione Tweve aliyepotea Zaidi ya miaka mitatu iliyopita katika kijiji cha
Igolwa kata ya Ipepo wilayani Makete mkoani Njombe imegundulika aliuawa (Zaidi
ya miaka 3 iliyopita) na kisha mwili wake kuzikwa na mtuhumiwa wa mauaji hayo
Tukio hilo la kusikitisha
linadaiwa kufanywa na Bw. Amini Sanga Ambapo
baada ya kubanwa na vyombo vya dola vilivyokuwa vikimhoji amekiri kuhusika na
mauaji hayo na kwenda kuonesha alipomzika marehemu ambapo baada ya kufukua
ilikutwa mifupa inayosadikika kuwa ni mabaki ya mwili wa marehemu huyo, eddy blog imejulishwa
Akizungumza na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa kijiji cha Igolwa bw. Batueli Tweve Amesema enzi za uhai wa
marehemu alikuwa akipasua mbao na mtuhumiwa na baada ya kipindi Fulani alipotea
na juhudi za kumtafuta hazikuzaa matunda hadi Alhamisi ya Desemba 14 mwaka huu
walipomtilia shaka mtuhumiwa na kumuweka chini ya ulinzi na baada ya mahojiano
ikabainika kuwa anahusika na mauaji ya marehemu huyo
Amesema chanzo cha mauaji hayo
kinadaiwa kuwa ni deni alilokuwa akilidai mtuhumiwa kwa marehemu huyo kiasi cha
shilingi 80,000 ambacho kilitakiwa kugawanywa nusu na kila mmoja apate shilingi
40,000 ambapo baadhi ya kauli zake alizokuwa akizitoa mtuhumiwa zilitiliwa
shaka na watu kabla ya ndugu wa marehemu kuzifuatilia kwa kina hali
iliyopelekea mtuhumiwa huyo kuwekwa chini ya ulinzi na kukiri kufanya mauaji
hayo kwa kutumia panga
Mwenyekiti huyo akiithibitishia eddy blog amesema baada ya
mtuhumiwa kufanya mauaji hayo aliupeleka mwili wa marehemu Umbali wa kilomita
moja kutoka eneo alimofanyia mauaji hayo na kuchimba shimo kisha kuufukia mwili
huo
“Ijumaa ya Desemba 15 mwaka huu
baada ya jeshi la polisi kupata kibali cha kufukua mwili wa marehemu walifika
kijijini hapa wakiongozana na mtuhumiwa na taarifa zikatolewa kwa kijiji kizima
tukaelekea eneo alipoufukia huo mwili na kutuonesha tuchimbe wapi, na kweli
baada ya kuchimba tuliukuta mwili wa marehemu lakini ilikuwa ni mifupa tu”
amesema Mwenyekiti huyo wakati anaongea na eddy blog
Hali hiyo imemlazimu daktari
aliyeongozana na jeshi la polisi kuchukua sehemu ya mabaki ya mwili wa marehemu
kwa ajili ya uchunguzi Zaidi
Jeshi la polisi limefika kijijini
hapo kwa hatua Zaidi za kisheria ambapo pia wanamshikilia mtuhumiwa huyo huku
familia ya marehemu ikifanya msiba baada ya kupata uhakika kuwa ndugu yao ni
marehemu baada ya kutoonekana kwa muda mrefu
Juhudi za kumpata kamanda wa
polisi Mkoa wa Njombe kuzungumzia tukio hilo bado zinaendelea