Hakimu mkuu katika mahakama ya Nairobi Bw Francis Andayi aliamuru daktari anayeshtakiwa pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Imenti ya Kati Gideon Mwiti afikishwe kortini Jumanne mnamo Desemba 19
Bw Andayi alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa kwamba Dkt David Muchiri anazuiliwa katika gereza kuu la Kamiti kwa mauaji ya wakili aliyekuwa anafanya kazi katika mamlaka ya ushuru nchini KRA.
Bw Andayi alikuwa ameaorodhesha kesi ya ubakaji dhidi ya Bw Mwiti kusikizwa jana lakini haingeza kuendelea kwa vile Dkt Muchiri anazuiliwa katika gereza kuu la Kamiti kwa kosa la mauaji.
Wakili Dkt John Khaminwa anayemwakilisha Bw Mwiti alimweleza hakimu kwamba “mshtakiwa wa pili (muchiri) hayuko kortini kwa vile anakabiliwa na shtaka la kumuua wakili.”
“Muchiri hajafikishwa kortini kutoka gereza kuu la Kamiti,” alisema Dkt Khaminwa.
“Natumai Bw Andayi ulisoma katika magazeti kwamba mshtakiwa wa pili (Muchiri) alishtakiwa kwa kumuua wakili wa KRA eneo la uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA). Hii kesi haiwezi kuendelea leo (Jumatatu). Nilifika mapema nikuombe utenge siku nyingine ya kusikizwa kwa kesi hii,” alisema hakimu alifahamishwa.
Kiongozi wa mashtaka Bw Daniel Karuri alithibitisha hayo na kuomba kesi hiyo itengewe siku nyingine.
Wiki iliyopita Bw Andayi alitupilia mbali ombi la Bw Mwiti la kutaka kesi inayomkabili itupiliwe mbali.
Mwiti amekanusha shtaka la ubakaji, kumpiga na kumuumiza mlalamishi na kumtisha mlalamishi.
Alikanusha kumbaka mwanamke katika Kilabu kilichoko barabara ya Woodvale Groove mtaani Westlands Nairobi mnamo Machi 15, 2015.
Dkt Muchiri alidaiwa alikuwa amempima mlalamishi kubaini ikiwa alikuwa na virusi vya Ukimwi.
Ikiwa atapatikana na hatia mshtakiwa atasukumwa jela kifungo cha miaka 10.
Bw Mwiti na Dkt Muchiri wako nje kwa dhamana ya Sh100,000.