CHADEMA yatoa msimamo viongozi wake kuhamia CCM

CHADEMA kupitia kwa Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema kimetoa msimamo wake juu ya baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao wamekuwa wakihama na kusema wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli

Mrema amesema kuwa viongozi hao wanapoondoka waseme sababu za kweli zinazowafanya kuondoka CHADEMA na kwenda CCM na si kuwadanganya wananchi kwa kutoa sababu zisizo na msingi ambazo ni uongo. 
"Leo tarehe 14 Disemba, 2017 tumepokea taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Mbunge wa Siha Dr.Godwin Mollel amejiuzulu uanachama na kujiunga na CCM. Dr.Godwin Mollel ameeleza sababu ya uamuzi wake huo ni kutaka kulinda rasilimali za Taifa. Sababu hii aliyoitoa ni ya kushangaza kwani Bunge ndicho chombo chenye wajibu wa kusimamia na kulinda rasilimali za Taifa kwa niaba ya wananchi" 
Mrema aliendelea kusema kuwa "Ni jambo la kushangaza kwa kuwa kitendo chake cha kulikimbia Bunge kama chombo cha kusemea na kutetea rasilimali za Taifa na kuja uraiani inatoa taswira gani maana kalikimbia Bunge lenye wajibu huo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu. Tunawashauri wale wote ambao wanajitoa waeleze sababu halisi na sio kuhadaa umma kwa sababu uchwara kama hizi, maana wapo wanaosema wanaacha kazi kwenda kuunga mkono dhana ya 'hapa kazi tu' na wengine wanasema wanaenda kuunga mkono juhudi za kuboresha maisha kwa kuacha kazi" 
Aidha Mrema alisema kuwa chama chao kipo imara na wataendelea na ajenda zao bila kuyumbishwa na wimbi la watu wachache ambao wamekuwa wakihama chama hicho kwa kutoa sababu nyepesi. 
"CHADEMA tuko imara sana na tutaendelea na ajenda zetu bila kuyumbishwa na wimbi hili la watu wachache ambao wameamua kuwasaliti wapiga kura wao kwa kutoa sababu zisizo za msingi ambazo hazina maslahi kwa Taifa bali kwa maslahi yao binafsi. Huu ni ubinafsi wa hali ya juu. Tutaendelea kujenga Taifa letu na Chama chetu bila kujali njaa za baadhi yetu wala maslahi ya watu wachache. Ila kwa hakika ni kuwa wale wenye dhamira thabiti ndio wataweza kufika mwisho wa safari ya kuleta mabadiliko salama. Ni dhahiri wale waliotanguliza ubinafsi hatutaweza kufika nao mwisho wa safari hii" 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo