Akizungumza na ITV Leo mhasibu huyo Bwana. Godfrey Gugai amesema kuwa taarifa zilizotangazwa za kuwa anatafutwa zimemsikitisha kwani yeye yupo nchini na hajatoroka kwenda mahala popote.
"Nimesikitika kwa sababu kwa taasisi kama TAKUKURU, taasisi yenye dhamana ya uchunguzi, sikutegemea kiongozi mwenye dhamana aseme kwamba nimekimbilia Congo, kwa sababu taasisi kama hiyo yenye dhamana ilikuwa na wajibu wakuangalia kwenye mipaka kama kweli nimekwenda nje ya nchi" Amesema Gugai.
Kuhusu tuhuma zilizotolewa dhidi yake amesema kuwa ameamua kufika makao makuu ya TAKUKURU ili kusudi suala hilo liweze kwenda Mahakamani kwa sababu mahakama ndio chombo pekee chenye kutoa haki.
"Tuhuma zimetolewa lakini nimeambiwa ni suala la kimahakama ndiyo maana nimeamua mimi mwenyewe kufika makao makuu ya TAKUKURU ili suala hilo liende mahakamani na kwakuwa mahakama ndiyo chombo chenye kutoa haki " Gugai amefafanua.
Kufuatia donge nono lililotangazwa siku ya tarehe 14 Nov 2017 na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Mbung’o kwamba atakaye fanikisha kukamatwa kwa mhasibu huyo Bwana Godfrey Gugai atapewa Milioni 10, mhasibu huyo amesema kuwa Mh. Rais wa Tanzania anamapambano ya kuminya matumizi ili kuleta huduma bora za afya kwa wananchini.
"Naomba uueleze umma asije akatokea mtu yeyote kwamba amenitafuta mimi ili apate hilo donge nono, hilo donge nono ninashauri litumike kwenye huduma muhimu za kijamii, kama sekta ya Afya wazipeleke huko zisaidie wananchi ambao wanahitaji huduma za Afya" Ameelezea Gugai.
Chanzo: ITV