Kumbe Nyalandu kawazidi Ujanja CCM

Na Balinagwe Mwambungu 

KUJIUZULU kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Lazaro Nyalandu, kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumetibua bahari na mawimbi makubwa yanapiga fukwe na walioathirika wanapiga kelele. 

Uliibuka mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, kuwa kulikuwa na kitu ‘nyuma ya pazia’ kutokana na utata wa taarifa kuhusu kujiuzulu kwake. 

Nyalandu alisema amemtaarifu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa barua huku Ofisi ya Spika ikisema tayari ilikuwa imepokea barua kutoka CCM ya kumfukuza uanachama Nyalandu. Wachambuzi wa mambo wanahoji kama ni kweli CCM wanawezaje kumfuta mtu uanachama bila kumpa nafasi ya kujieleza? Halafu wanasema chama hicho kinafuata misingi ya kisheria. 

Je, kwa mfano Nyalandu akienda mahakamani (haitatokea) na kudai haki yake ya asili (natural justice) itendeke! Hoja nyingine ambayo ni muhimu ijibiwe ni kuhusu tamko la Ofisi ya Spika, haikuweka wazi barua ipi ilifika kwanza; ya Nyalandu au ya CCM. Na kama ya Nyalandu ilitangulia, kwanini Spika alimwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, akisema Nyalandu amefukuzwa uanachama na si kwamba Nyalandu amejitoa CCM! Je, ina maana Ndugai anapokea maelekezo kutoka CCM ili afanye uamuzi? Katika hali hiyo hiyo, ina maana Nyalandu alijua kulikuwa na kikao cha siri ambacho kilikuwa kinamjadili na akatonywa uamuzi uliofikiwa. 

Ili kuwanyima CCM hadhi (credibility), akatangaza kujiuzulu kabla ya CCM kuandika barua. Swali jingine ni je, CCM walimpa barua ya kumfukuza Nyalandu? Haya ni maswali madogo, lakini yanawaumbua CCM kwamba si wakweli, wanatenda mambo kwa hila na wanakandamiza uhuru wa wanachama wake. 

Barua ya CCM kwenda kwa Spika, haifafanui ni mambo gani ambayo Nyalandu aliyafanya ambayo adhabu yake ni kufukuzwa uanachama. Haitoshi kusema kwamba chama kimechukua hatua za kinidhamu dhidi ya mbunge wake na kuacha wanachama wengine midomo wazi. 

Ni mambo gani ambayo Nyalandu alifanya kinyume na mwenendo na maadili ya chama chake? Wachamuzi wa mambo wanasema Nyalandu aliwahi kutamka kwamba, anakusudia kupeleka muswada bungeni kuomba Bunge la Katiba lirejeshwe na kujadili mapendekezo ya Tume ya Warioba. Je, hili ni kinyume na msimamo wa CCM? Kama ndivyo, wananchi waelewe kuanzia sasa CCM wanapinga matakwa yao kudai Katiba mpya. 

Halafu barua yao kwa Spika inasema Nyalandu amekuwa akienda kinyume cha filosofia na itikadi ya chama; filosofia na itikadi ya CCM ni ipi, maana mambo muhimu yanayotamkwa ni kusema ukweli, kutokula rushwa na kutofitini watu. Ni lipi katika haya aliyafanya Nyalandu? Nyalandu mwenyewe alisema ameamua kujiondoa CCM kwa sababu Bunge ambalo lina wanachama wengi wa chama hicho limeshindwa kuisimamia Serikali, anapinga vitendo vya ukandamizaji wa haki za binadamu na kutoheshimu mipaka ya madaraka ya Bunge na Mahakama. 

Je, Chama Cha Mapinduzi kinayakumbatia haya? Hizi ndizo hoja ambazo CCM wanatakiwa kuzijibu. Lakini wachambuzi wa mambo wanasema kuwa wanaosema Nyalandu ni fisadi na yuko chini ya uchunguzi, wanafanya hivyo kufurahisha watu. Kama ni ufisadi umetamalaki CCM. 

Kumbukeni kashfa zote kubwa; EPA, Tegeta Escrow, Loliondo, Richmond, Meremeta, Minofu ya Samaki, Uingizaji wa Sukari kinyume na sheria na nyinginezo, zimetendeka katika utawala wa CCM. Kama CCM walikuwa wanajua kuwa Nyalandu ni mwizi, walimvumilia kwa sababu ni mwizi mwenzao; mmoja wao anapotoka katika kundi la wezi, wanaogopa kuwa atawaumbua. 

Nyalandu amekuwa kiongozi ndani ya CCM kwa miaka takriban 17, hakuna aliyemnyooshea kidole, anatangaza kujivua gamba watu wanapiga kelele! Mtu mmoja aliandika hivi kwenye mtandao: ‘Kati ya makosa ambayo hutakiwi kufanya ni kumtukana mtaliki wako.’

 Nyalandu hajamtukana mtu, ila watesi wake ndani ya CCM wamepata nafasi ya kubwata. Nyalandu kama kiongozi wa juu asingeweza kuondoka CCM bila kueleza sababu. 

Anasema Nyalandu ameeleza sababu ya kukitaliki CCM, basi nacho kieleze yake si kusema mambo kijumla jumla, eti amekwenda kinyume cha filosofia na itikadi ya chama ndiyo sababu ya kumfukuza! Anikeni ukweli. 

Mwananchi mwingine aliandika kwenye mtandao: “Wakiwa kwenu kimya! Wakitoka visasi vinaanza. CCM wanalazimika kufuata mfumo mbovu. Sasa mnatuzuga mnaboresha…ila sisi wananchi tumechoka na mfumo wa kubebana. Mkuu anasema majizi yote yanakimbilia Chadema. 

Kumbe majizi yanafahamika, mnasubiri nini kuyaondoa. Mnasubiri mpaka wajiondoe ndio mseme.” Watu wenye akili wanajua kuwa siasa chafu zinaendeshwa CCM. Wanagombea nafasi za uongozi ili nao wale. Ujio wa Mwenyekiti mpya wa CCM, John Pombe Magufuli, umewatikisa. Nyalandu ametangulia, wengi wanajiandaa kutimka. Tusubiri. *0757-262672

Chanzo: Gazeti Mtanzania


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo