Aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula amesema licha ya jina lake kuenguliwa katika kugombea uenyekiti wa chama hicho, hana mpango wa kukihama chama cha Mapinduzi
Ndugu Chaula ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa chama hicho muda mchache kabla ya kujiuzulu nafasi hiyo kupisha uchaguzi ufanyike wa kumpata mwenyekiti mpya, ambapo amesema pamoja na figisu alizofanyiwa na baadhi ya watu lakini "hatoki mtu hapa" akimaanisha hatakihama chama cha Mapinduzi
"Naombeni mseme kama nayosema mimi, nikisema hatoki mtu hapa na nyie muitikie hivyo hivyo, maana kuna watu wanafikiri wakinifanyia figisu ndio nitaondoka CCM sasa nawaambia hivi, haondoki mtu hapa" amesema Chaula
Alitumia muda huo pia kuelezea aliyoyafanya ndani ya chama tangu aingie madarakani 2012 kuwa ni pamoja na kufanikisha ujenzi wa ofisi mpya za CCM wilaya ambazo zimeanza kutumika, kutembelea kata zote za wilaya ya Makete kusikiliza kero za wanachama, kutumia fedha zake binafsi kufanikisha shughuli za chama
Jana Novemba 25, Onna Nkwama alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa 4 wa chama hicho wilaya akimrithi Francis Chaula aliyemaliza muda wake
Tangu wilaya ya Makete kuanzishwa chama cha mapinduzi kimeongozwa na wenyeviti wanne ambao ni Amosi Sukunala Nkwama, Jasel Mwamwala, Francisa Chaula na sasa ni Onna Nkwama