Kamati ya ulinzi na usalama wilayani Bagamoyo imesema kuwa inafanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha vifo vya walimu wawili katika halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani ambao waliuwawa kwa nyakati tofauti
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majidi Mwanga amesema kuwa Kamati ya ulinzi na usalama inachunguza juu ya vifo vya walimu hao wawili waliouwawa mwezi Septemba na kusema watu waliotenda jambo hilo wakipatikana watapelekwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
"Suala hili linafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na ustadi wa hali ya juu na askari wa jeshi la polisi lakini bado tunaendelea kupokea taarifa zozote kwa watu ambao wanafahamu juu ya jambo wazifikishe taarifa polisi ili tuweze kubaini na kuwakamata watu waliotenda uhalifu huo wa kuwauwa walimu wetu" alisema Mwanga
Mwalimu wa shule ya msingi George Mbalala na Mwalimu Abdala Salumu wa shule ya sekondari katika Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani kwa nyakati tofauti mwezi Septemba waliuawa na watu wasiojulikana, mmoja kwa kuvamiwa na mwingine kwa kuchomwa kisu akiwa nyumbani kwake.