Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba amesema wakati wakiwa katika kampeni ya kuhamasisha uhuru wa habari na kujieleza, yanayoendelea sasa yanawarudisha nyuma.
Amesema hayo leo Jumanne alipotakiwa na Mwananchi kutoka maoni kuhusu kufungiwa gazeti la Tanzania Daima.
“Hatujui Serikali inataka kubaki na gazeti moja au la, kufungia gazeti si suluhisho, kama gazeti limekosea kwa nini wasikae na kuona jinsi ya kulimaliza, kufungia unawanyima wananchi haki ya kupata habari,” amesema Dk Kijo Bisimba.
Hakuwa pekee yake mwenye msimamo kama huo.
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema, “huu ni ukatili dhidi ya magazeti na vyombo vya habari kwa jumla, hakuna nia njema kwa kuwa fungia fungia imetawala na haina nia njema hata kidogo.”
Meena amesema hata kama gazeti limekosea basi adhabu ingeweza kuwa hata wiki moja lakini kufungia siku 90 inasababisha familia za wafanyakazi kuyumba, Serikali kukosa mapato na huenda mara baada ya adhabu hiyo kumalizika wanaweza wasirudi sokoni.
“Watafungia yote watabaki na wanayoyapenda, huu ni ukatili mkubwa. Tutakutana kuona hatua za kuchukua lakini hatuko salama,” amesema Meena.
Serikali katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Dk Hassan Abbasi imesema imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Tanzania Daima kwa muda wa siku 90 kuanzia leo Jumanne Oktoba 24,2017.
Imesema agizo pia linahusu toleo la mtandaoni la gazeti hilo.
Dk Abbasi amesema uamuzi huo unatokana na makosa makubwa katika toleo namba 4706 la Oktoba 22, 2017 likiwa na habari ya uongo kuwa, “Asilimia 67 ya Watanzania wanatumia ARVs.”
Amesema habari hiyo imeupotosha umma kwa kiasi kikubwa na kuleta taharuki, huku ikikiuka kifungu cha 54(1) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016.
Mkurugenzi huyo amesema Mhariri wa Tanzania Daima alikiri kosa na kuomba radhi kwa upotoshaji uliofanywa katika habari hiyo.
“Hata hivyo, pamoja na kuomba radhi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ametumia mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari, baada ya jitihada na juhudi za muda mrefu za Serikali kuwashauri na kuwakumbusha wahariri wa gazeti hili kuhusu wajibu wa kufuata misingi ya taaluma na sheria,” amesema.
Dk Abbasi ametoa mifano kadhaa ya makosa ya hivi karibunin ya gazeti hilo. Serikali imewakumbusha wana tasnia ya habari kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na yenye wajibu, misingi na maadili.