Viapo Mbela ya rais Magufuli IKULU leo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Oktoba 2017 amewaapisha Wakuu wa Mikoa 6, Makatibu Wakuu 4 na Naibu Makatibu Wakuu 7 aliowateua jana tarehe 26 Oktoba, 2017.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wengine mbalimbali.
Wakuu wa mikoa walioapishwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. Adam Kighoma Malima, Mkuu wa Mkoa Manyara Bw. Alexander Pastory Mnyeti, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Joackim Leonard Wangabo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Robert Gabriel Lughumbi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Gasper Byakanwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Christina Solomon Mndeme.
Awali Bi. Christina Solomoni Mndeme aliapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na baada ya kiapo Mhe. Rais Magufuli amefanya mabadiliko kwa kumhamisha kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amehamishwa na sasa atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Makatibu Wakuu walioapishwa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhandisi Joseph Kizito Malongo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Paul Mlawi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Dorothy Stanley Mwanyika na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Samwel Msanjila.
Naibu Makatibu Wakuu walioapishwa ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Dorothy Aidan Mwaluko, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Bi. Butamo Kasuka Phillip, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Thomas Didimu Kashililah na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Utawala) Bi. Susana Bernard Mkapa.
Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Biashara na Uwekezaji) Prof. Joseph Rwegasira Bushweishaija, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Niclolaus William na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Viwanda) Bw. Ludovick James Nduhiye.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi hao kuwatumikia wananchi vizuri kwa kutatua kero zinazowakabili na kuleta mabadiliko yatakayosaidia kuboresha maisha yao.
Ametolea mfano wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kuwa hatarajii kusikia wanafunzi vyuo vya elimu ya juu wamecheleweshewa mikopo kwa kuwa tayari Hazina imeshapeleka Shilingi Bilioni 147 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi ambao vyuo vinafunguliwa hivi karibuni.
“Nataka kila Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ajiulize amefanya nini kubadili maisha ya wananchi wa Mkoa wake ama Wilaya yake, nataka Makatibu Makuu na Naibu Makatibu Wakuu wakatatue kero zilizopo katika wizara zao” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda kufanya mabadiliko ya kiutendaji katika Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri diplomasia ya uchumi, kuhakikisha kila Balozi anayeiwakilisha Tanzania nje ya nchi anafanya kazi yenye kuleta manufaa kwa Tanzania na kuondoa watumishi wa waliopo katika Balozi mbalimbali duniani pasipo sababu za msingi za kuwepo kwao nje ya nchi.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Oktoba, 2017
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Adam Kigoma Malima kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 28, 2017 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Alexander Pastory Mnyeti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 28, 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe.Bi. Christine Solomon Mndeme kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kabla ya kumbadilisha na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, kubadilishana na Dkt. Bilinith Mahenge anayehamia Dodoma Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 28, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Thomas Didimu Kashililah kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya KilimoIkulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 28, 2017 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Nicholaus B. William kuwa Naibu Katibu Mkuu   Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 28, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma na Katibu Mkuu kiongozi wakiwa katika picha ya kumbukumbu na viongozi wa mbalimbali pamoja na wale aliowaapisha Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 28, 2017, PIcha na IKULU


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo