
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Loota Sanare wakati wa uchaguzi wa viongozi wa CCM Wilaya uliofanyika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Monduli. Wanachama hao kwa kauli moja walisema wamedhamiria kulikomboa jimbo hilo ambalo kwa sasa linaongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Sanare alisema hakuna asiyejua kuwa Wilaya ya Monduli inaangaliwa kwa jicho la kipekee kwa sababu ya mambo mbalimbali ya kisiasa ikiwemo ya vyama na makundi, lakini baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuhamia Chadema kugombea Urais, baadhi ya wanachama walihama naye na kusababisha misukosuko ndani ya CCM.
Alisema lakini kwa kuwa CCM ipo imara, wamejipanga kuondoa mamluki ndani ya chama hicho kwa kuchagua viongozi bora watakaowezesha jimbo hilo kurudi CCM. “Lowassa aliletea misukosuko kabla ya kuhama chama kwa sababu alikuwa akitaka wagombea fulani ndiyo wawe viongozi, lakini hivi sasa hakuna hilo hatutaki mamluki ndani ya chama chetu ndiyo maana amehama na 2020 tutalichukua jimbo hili ,” alieleza Sanare.