Mwanamke mmoja Christina Mbilinyi anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi
ya miaka 70 mkazi wa kijiji cha Lupalilo wilayani Makete mkoani Njombe amekutwa
akiwa amekufa katika mto kijijini hapo
Tukio hilo la kupatikana akiwa amefariki dunia limegundulika leo baada
ya taarifa za kupotea kwake kutolewa kijijini hapo tangu jumamosi, lakini leo
wanakijiji wakaamua kuendesha msako wa kuanza kumtafuta katika maeneo aliyopita
wakati anaondoka
Akizungumza na mwandishi wetu ndugu wa karibu wa Marehemu alikokuwa
akiishi kijijini hapo amesema Ijumaa ya Septemba 29 mwaka huu Marehemu aliaga
kuwa anakwenda kusalimia ndugu zake waliopo katika kijiji cha Usagatikwa na alifika
kwa ndugu zake hao
Amesema Septemba 30 marehemu huyo aliondoka kwa ndugu zake wa
Usagatikwa kurudi nyumbani anakoishi Lupalilo lakini hakufika nyumbani kama
ilivyotarajiwa hali iliyowapa mashaka na kuanza kumtafuta kabla ya kukutwa
akiwa amefariki katika mto huo
Diwani wa kata ya Lupalilo Mh Imani Mahenge naye amezungumzia tukio
hilo kwa kusema baada ya kumpata mkazi huyo akiwa amefariki alitoa taarifa kwa jeshi la polisi
Jeshi la polisi wilaya ya Makete limefika eneo la tukio kwa ajili ya
kukamilisha taratibu zao kwa mujibu wa sheria, ambapo baada ya uchunguzi ndugu
wamekabidhiwa mwili wa marehemu kwa ajili ya maziko









