MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika shule moja ya sekondari Wilaya ya Kinondoni jijini, Samuel Wilson, Jumanne iliyopita, saa mbili usiku, alifunga mtaa maeneo ya Mwenge Mlalakuwa na kuwachoma visu watu kadhaa akiwemo Paulo Ndensai na Yasin Mohammed.
Akisimulia kwa uchungu tukio hilo mmoja wa mashuhuda alisema mwanafunzi huyo alikuwa akimpiga kijana mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Mohammed huku akimchoma kwa kisu alichoshika hali iliyowafanya wananchi waliokusanyika eneo hilo kukimbia kwa kuhofia usalama wao.
Shuhuda huyo alisema denti huyo akiendelea kumshambulia Mohammed ambapo chanzo cha ugomvi huo hakijawekwa bayana, kaka yake Mohammed aitwae Paulo Ndensai alitokea na kwenda kumuokoa mdogo wake.
“Katika harakati za kumuokoa mdogo wake, mtuhumiwa alimuacha aliyekuwa akimshambulia na kuhamishia varangati kwa kaka mtu ambapo alimchoma kwa kisu kichwani juu kidogo ya sikio la kushoto, kingine akamchoma kichwani juu, hali iliyofanya achuruzike damu nyingi,” alisema shuhuda huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Aliongeza kuwa Ndensai baada ya kuona anachomwa visu sehemu mbalimbali za mwili wake, alinyoosha mikono ili kujikinga na kisu kilichokuwa kikimuelekea utosini ambacho kilimjeruhi mkononi.
“Yaani bila kujikinga na kile kisu alichonielekeza utosini sasa hivi tungekuwa tukisema mengine,”alisema Ndensai huku akiwa amejinyoosha kwenye kochi kwa madai kuwa ana kizunguzungu kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Baada ya kutujeruhi na hali zetu kuwa mbaya, alituacha tukitapakaa damu ambapo mimi nilipoteza fahamu na kuzinduka baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo nilipelekwa na wasamaria wema nikapatiwe hati namba 3 ya polisi (PF3) kwa ajili ya kutibiwa.
“Tukiwa kituoni nilitoa maelezo ambapo mtuhumiwa alifunguliwa kesi kwenye jalada lenye namba UD/ RB/4418/2017 ambapo alitakiwa kukamatwa lakini mpaka sasa bado hajakamatwa.
“Kila tukienda kituoni askari tunaowakuta wananiambia niwatafutie Bajaj na hata nikiwaambia sina pesa ya kukodi Bajaj wananiambia hawawezi kwenda kunikamatia mtuhumiwa wangu.
“Kutokana kukosa pesa ya kuwapa wakodi hiyo Bajaj, mtuhumiwa wangu anaendelea kututambia mtaani hali inayotupa wasiwasi wa kuweza kutushambulia tena.” Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Muliro Jumanne Muliro hakupatikana jana kufafanua tatizo hilo.
STORI: RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY