Mahakama: Manji Arudishwe Polisi

Na Karama Keyunko,Blogu ya jamii.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, imeruhusu mfanyabiashara Yusuf Manji na wenzake watatu kupelekwa polisi na kuhojiwa dhidi ya kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili ili kukamilisha upelelezi.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi kufuatia barua ya maombi kutoka kwa Mkuu wa upelelezi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, (ZCO), ndipo akaandika hati ya kuwatoa washtakiwa mahabusu (remove order) ili kuwafanyia mahojiano katika kesi namba 33/2017

Amesema hawawezi kukataa maombi hayo ya polisi kwani kufanya hivyo ni sawa na kupingana na kauli ya mahakama ya kukamilisha upelelezi, na ndio maana ikatolewa hati ya kuwatoa mahabusu kwa ajili ya mahojiano. “Hii sio mara ya kwanza kuwatoa washitakiwa kwa upelelezi," alisema Hakimu Shaidi.

Aidha amewaagiza polisi kuhakikisha washtakiwa wanatendewa ikiwemo kuzingatia afya zao kwani wanawakabidhi wakiwa na afya nzuri na kama watahitaji uwakilishi wa mawakili wao wapate uhuru wa kuwakilishwa kwenye jambo lolote na isiwe kificho.

Hakimu Shahidi amesema, "Namkabidhi Koplo Dotto kama barua inavyoelekeza kuwa nimkabidhi Sajenti Mkombozi au Doto lakini kwa kuwa Mkombozi hayupo basi namkabidhi Doto ila washitakiwa warudishwe kesho ndani ya muda wa kazi.

Mbali na Manji, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), Mtunza stoo, Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43)  mkazi wa Chanika wanakabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.

Mapema, akiwasilisha maombi hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi aliiomba mahakama iruhusu washitakiwa waweze kukabidhiwa kwa Polisi ili kutimiza matakwa ya upelelezi ambapo amedai kifungu
Cha 59 cha CPA kinawapa mamlaka Polisi kufanya upelelezi.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Hudson Ndusyepo alipinga watuhumiwa kwenda kuhojiwa kwa madai kuwa, mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri hiyo sababu DPP hajatoa Kibali kwa mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo zaidi ya kutaja tarehe, alidai mahakama hiyo imefungwa mikono ya kutoa amri dhidi ya maombi hayo au yoyote yale.

Naye wakili Hajra Mungula aliiomba mahakama kukataa ombi hilo kwa madai kuwa washitakiwa hao wako chini ya ulinzi na kwamba upande wa mashitaka uliwashitaki washitakiwa kwa mbwembwe na kuwasilisha hati ya kuwazuia dhamana huku wakijua kwamba hawajakamilisha upelelezi

Hata hivyo, Wakili Kishenyi alidai mahakama imekuwa ikisisitiza kukamilisha upelelezi na kwamba wanachofanya ni sehemu ya kukamilisha upelelezi.
Pia alidai washitakiwa hao wanahaki ya kuwakilishwa hivyo maombi yao yakubaliwe.

Washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa na sare za na vifaa mbali mbali vya jeshi.
Mfanyabiashara Yusuph Manji, akitoka Mahakamani baada ya Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi kuruhusu yeye na wenzake watatu wanaokabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi kupelekwa polisi kuhojiwa ili kukamilisha upelelezi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo