Msemaji wa Serikali Dk Hassan Abbasi amesema kwamba kuanzia leo hadi Oktoba 15, Magazeti yote yataanza kusajiliwa upya.
"Baada ya Oktoba 15, 2017 hakuna atakayeruhusiwa kuchapisha bila usajili"Amesema Dk Abbasi na kuongeza;
"Mfumo mpya wa utoaji wa leseni kwa machapisho yote umeanza rasmi leo ‘’
Amesema taratibu zote za upatikanaji wa leseni zimewekwa katika tovuti http://www.maelezo.go.tz "-
Mawasiliano kwa ajili ya ufafanuzi kuhusu utaratibu wa usajili ni 0622664606 na 0717312417 au kupitia maelezo@habari.go.tz
==
==
KUANZA UTOAJI WA LESENI KWA MAGAZETI
NA MAJARIDA
Dar es Salaam, Agosti 23, 2017:
SERIKALI
kupitia Idara ya Habari (MAELEZO) inapenda kuutaarifu umma kuwa katika
utekelezaji wa matakwa ya kifungu cha 5(e) cha Sheria ya Huduma za Habari,
2016, itaanza kutoa leseni za machapisho mbalimbali ikiwemo magazeti na
majarida yote nchini.
Utoaji
wa leseni hizo pia ni kwa mujibu wa Kanuni ya 7 ya Kanuni za Sheria ya Huduma
za Habari za mwaka 2017 zilizochapishwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na 18
la Februari 3, 2017.
Kwa
mujibu wa sheria, utaratibu wa sasa unafuta mfumo wa awali wa utoaji wa Hati za
Usajili wa magazeti na majarida uliokuwa ukitumika kwa mujibu wa Sheria ya
Magazeti ya mwaka 1976 ambayo kwa sasa imefutwa.
Aidha
utaratibu huu mpya utawahusu wamiliki wote wa magazeti (newspapers), majarida
(journals, magazines na newsletters) na wamiliki wapya ambao hawakuwa
wameyasajili machapisho yao. Aidha leseni hizi zitahuishwa kila mwaka kwa
mujibu wa Kanuni za 8(3) na 12(1)(2) za Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari,
2017.
Fomu za maombi
pamoja, akaunti ya kulipia na orodha ya nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya
usajili vinapatikana kuanzia leo katika ofisi za MAELEZO Dar es Salaam na
Dodoma au katika sehemu ya “Huduma Zetu” katika tovuti yetu: www.maelezo.go.tz.
Kwa wamiliki wa magazeti na majarida ambao wana
usajili wa zamani, Serikali inatoa fursa
kuanzia
leo mpaka Oktoba 15, 2017 wawe wamekamilisha taratibu na kupatiwa leseni
mpya za uendeshaji na uchapishaji wa majarida na magazeti na baada ya muda huo
hawataruhusiwa kuyachapisha kwani watakuwa wametenda kosa kisheria.
Kwa ufafanuzi zaidi kuhusu utaratibu wa usajili, wasiliana
nasi katika namba 0622 664606 na 0717 312417, tembelea tovuti yetu au wasiliana
nasi kupitia: maelezo@habari.go.tz
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi Mkuu,
Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.