Muuguzi anayefanya kazi Kituo cha Afya Kata ya Igurubi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Damian Mgaya (26) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma ya kumbaka binti wa miaka 18 mkazi wa kitongoji cha Mwagala B, Kijiji cha Mwagala.
Mtendaji wa Kata ya Igurubi, Ntemi James alisema uhalifu huo umefanyika Julai 14, mwaka huu saa 8 usiku hadi alfajiri wakati binti huyo akimuuguza mama yake, Tatu Simbi ambaye amelazwa katika kituo hicho cha afya baada ya kushambuliwa kwa kipigo na mume wake.
James alidai mtuhumiwa alimpokea mama wa binti huyo akiwa hoi na ndipo alimpatia matibabu kisha kumlaza katika kituo hicho cha afya huku akimchoma sindano ya usingizi ambayo ilisababisha mama huyo kupitiwa na usingizi.
Mtendaji huyo alidai kuwa muuguzi Damian alipoona mama wa binti huyo amelala, alimwambia waende wote chumba kingine ili akachukue dawa ya mama yake; lakini hata hivyo hakumpa dawa na badala yake alimwambia amchome sindano ili asipate maradhi kwa kuwa mazingira ya hospitali sio mazuri.
Baada ya kuambiwa hivyo, binti huyo alikubali kuchomwa sindano mbili na alipochomwa sindano ya kwanza aliishiwa nguvu na alipochomwa sindano ya pili alianguka na kupitiwa na usingizi hadi asubuhi.
Alisema baada ya kuona amelala pasipokuwa na fahamu, muuguzi huyo alianza kumbaka hadi alfajiri alipoamshwa na mama yake huku yeye akiwa hajitambui kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia sehemu zake za siri na mwili wote.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bonaventura Kalumbete alithibitisha kubakwa kwa binti huyo na muuguzi huyo na kueleza kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, alituma timu ya wataalamu ambayo ilibaini binti huyo kubakwa na amelazwa kwenye kituo hicho na hali yake ni mbaya kwani hawezi kutembea.
Aidha, Dk Kalumbete alisema uchunguzi wa awali unaonesha binti huyo alichomwa sindano wakati alikuwa hata haumwi na hizo dawa nazo zimechangia kumsababishia kushindwa kutembea huku akiahidi kuwa baada ya uchunguzi, muuguzi huyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, John Mwaipopo alikiri kukamatwa kwa muuguzi baada ya kupokea taarifa ya kubakwa kwa binti huyo, alimwagiza Mkuu wa Polisi Igunga kumkamata muuguzi huyo Damian Mgaya ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.