Kiongozi mmoja wa Yanga ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema mwanzoni walikuwa wakisuasua kuhusiana na kumsajili Himid kutokana na kuwa na uhakika wa kusajili Mkude ambaye alikuwa akishawishwa vilivyo na Ibrahimu Ajibu, lakini dili lake limebuma.
“Hatuna kingine cha kufanya isipokuwa kilichobakia ni kumsajili Mao na aliomba tumpatie Sh milioni 60 na mshahara wa Sh 3,000,000.
“Kwa hiyo inatubidi tufanye hivyo kwani awali tulikuwa tunamvizia Mkude ambaye alikuwa anataka milioni 50 lakini Simba wametuzidi ujanja, hivyo ni lazima Mao tumsajili sasa,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza:
“Mpaka kufikia sasa, kila kitu kipo tayari na tunachosubiri ni yeye kuja tu kusaini, kwa hiyo muda wowote mambo yanaweza kuwa safi.”
Endapo Yanga itafanikiwa kumsajili Himid itakuwa imepata kiungo mkabaji sahihi kwani kwa muda mrefu ilikuwa ikisumbuliwa na hilo, tangu alipoondoka Frank Domayo.