Dar es Salaam. Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limeaalani kitendo cha udhalilishaji kilichofanywa na Spika wa Bunge, Job Ndugai cha kumtoa kwa nguvu jana Waziri Kivuli wa Wizara ya Madini na Nishati, John Mnyika.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi na Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi wakati akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya chama hicho Kinondoni.
Katambi amesema Ndugai hakutumia busara kumtoa Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba, bali alikuwa na jazba katika kutoa uamuzi huo wa mbunge.
“Adhabu ya Mnyika kutoka nje ya Bunge ilitosha kabisa. Lakini si kumwambia asihudhurie vikao kwa siku kadhaa,” amesema Katambi.
Amesema ni wakati mwafaka wa Ndugai kufanya upya marejeo ya uamuzi aliyoutoa ambao kwa anadai ulikuwa wa jazba kuliko busara.
Hata hivyo, Katambi amesema vita ya madini haiwezi kufanikiwa kwa kuwatoa wapinzani nje ya Bunge ambao wana mawazo mbadala ambayo yanaweza kuwasaidia kwa namna moja au nyingine.
“Tunasikitika na kitendo kilichofanywa na Ndugai, nadhani busara alizisahau nyumbani basi angejaribu hata kuzikumbuka kuliko kutoa uamuzi kama ule."