Na Tiganya Vincent, RS- Tabora,31 Mei, 2017
Jumla ya shilingi milioni 180 zimekusanywa na Jeshi la Polisi mkoani Tabora katika kipindi cha Mwezi huo kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa na waindeshaji wa vyombo vya moto.
Takwimu hizo zilitolewa jana mjini Tabora na Kamanda wa Mkoa wa Tabora Wilbroad Mtafungwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari ofisi kwake wakati akitoa ufafanuzi juu ya jitihada mbalimbali wanazozifanya katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu mkoani humo.
Alisema makusanyo hayo yametokana tozo kwa madreva wa magari, pikipiki na bajaji na waendesha baiskeli walivunjia Sheria za Usalama barabarani katika kipindi hicho.
Kamanda alitaja baadhi ya makosa ni madereva wa Bodaboda kutovaa kofia ngumu wao na abiria wao , madereva wa magari kuendesha bila kuwa na leseni, mwendokasi, kutozingatia alama za barabara na kupakia abiria zaidi ya uwezo wa chombo cha usafiri.
Kamanda Mtafungwa alitoa wito kwa watu wote wanaoendesha vyombo vya moto Mkoani Tabora kuepuka kuvunja Sheria za Usalama Barabarani ili waokoe fedha wanazozipata zitumike kusaidia familia zao katika matumizi mengine ya maendeleo badala kulipa faini.
“Naomba waendeshaji wa vyombo vya moto kuzingatia Sheria za Usalama barabarani ili wasipigwe faini ambazo zinawafanya watoe fedha ambazo zingewesaidia wao na familia katika shughuli mbalimbali” alisema Kamanda huyo wa Mkoa wa Tabora.
Aidha , alitoa wito kwa vijana wote wanaoendesha Bodaboda na baiskeli maarufu kama daladala kujisajili katika vituo(vijiwe) na kukaa katika maeneo yao waliopagwa na viongozi wao ili kuwasaidie kuwafichua baadhi ya Wahalifu kujificha katika usafiri huo.
Kamanda Mtafungwa alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwabaini baadhi ya wahalifu ambao wanapenda kujificha katika kazi hiyo kwa kutokubali kukaa eneo moja kwa hofu ya kubainika uovu wao.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Mkoani Tabora linawashikilia watu sita wakiwemo madereva wa bodaboda wawili kwa tuhuma za kuvunja nyumba usiku na kuiba na wengine kununua mali inayodhaniwa ni ya wizi.
Kamanda Mtafungwa alisema kati ya watuhumiwa hao wanne walikiri kuhusika na uvunjaji nyumba na kuiba mali na wengine wawili walikutwa na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi.
Aliwataja waliokamatwa kwa tuhuma za kuvunja nyumba ni Issa Maganga(27), Salum Maganga(19), Hamis Malale(24) na Amri Salum (20) wote wakazi wa Ipuli katika Manispaa ya Tabora .Kamanda Mtafungwa aliongeza kuwa walikutwa na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi ni kuwa nia Maganga Salum(28) na Hussein Salum (28) wote wakazi wa Kiloleni Manispa ya Tabora.
Alivitaja vitu vilivyokamatwa ni pamoja na tairi za baiskeli 21, mzani mmoja na mawe yake, mikasi saba ya baiskeli , minyororo nane ya baiskeli, televisheni mbili inchi 32 , solar inchi 24 na kandambili jozi saba.
Vingine ni sigara pakiti 20 , Betri za radio jozi 18 , dawa za meno aina ya Whitedent na mafuta ya kujipaka.Alisema kuwa watuhumiwa hao walishindwa kudhibitisha uhalali wa mali hizo na hivyo nao wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani wakajibu makosa yanayowakabili.
Kamanda huyo alitoa wito kwa vijana mkoani Tabora kuacha kujiingiza katika vitendo vitakavyosababisha kukamatwa na hatimaye kupelekwa Mahakamani na kuongeza kuwa ni vema wakashiriki katika shughuli mbalimbali kama vile kilimo cha bustani ili kujipatia kipato halali badala ya kufikia kuvunja nyumba na maduka ya watu wengine.