Prof Lipumba avitaka Vyombo Vya habari Viisusie CUF ya Maalim Seif

Katika hali isiyo ya kawaida, Baraza Kuu la Uongozi linalotambuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, limetangaza rasmi kumvua madaraka Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sherif Hamad na kumtaja Magdalena Sakaya kuwa Kaimu Katibu Mkuu, na kwamba atafanya kazi zote za Katibu Mkuu.
Sambamba na hilo, limevitaka vyombo vya habari kuacha kuwaalika viongozi wa CUF wanaodaiwa kuvuliwa madaraka na Prof. Lipumba, na kutoa wito kwa vyombo vya dola kuchukua hatua kwa wale wote watakao fanya hivyo, kwa kuwa ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa kifungu cha 8B (2) sura ya 258 kinachoeleza kuwa mtu yeyote ambaye sio kiongozi wa chama haruhusiwi kufanya shughuli yoyote kama kiongozi wa chama hicho.
Wakati akisoma maazimio ya kikao cha baraza hilo, kilichofanyika Machi 25 na 26, 2017 kwenye ofisi ndogo za makao makuu ya CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumba amedai kuwa Maalim Seif amevuliwa wadhifa huo baada ya baraza hilo kujiridhisha kwamba ameshindwa kutimizia majukumu yake.
“Baraza kuu limesikitishwa na kukasirishwa na vitendo vya katibu mkuu kuhujumu chama na kupandikiza chuki dhidi ya mwenyekiti wa Taifa miongoni mwa wanachama wa CUF. Tangu septemba 24, 2016 hajafika ofisini na kukaidi wito wangu wa kuja ofisini kutekeleza majukumu yake kikatiba. Baraza kuu limeagiza kwamba katiba ya chama iheshimiwe na kutekelezwa,” amesema.
Licha ya baraza hilo kudai kumvua madaraka Katibu Mkuu, limewathibitisha wakurugenzi wapya walioteuliwa na Lipumba,limejaza nafasi za baraza kuu zilizowazi, uteuzi wa bodi mpya ya wadhamini wa chama, uteuzi wa wagombea wa bunge la afrika mashariki na kuthibitisha uteuzi wa mwenyekiti wa wajumbe wa kamati ya maadili.Hali kadhalika limeiagiza benki ya NMB kuzifungua akaunti za wilaya za chama hicho zilizofungwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF.
Wakati hayo yanajiri, upande wa Maalim Seif ukiwakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawalisiano na Umma CUF, anayedaiwa kuvuliwa wadhifa huo na Lipumba,Mbarala Maharagande  amesema hawatambui maazimio ya baraza hilo kwa kuwa si halali huku akisisitiza kuwa viongozi wanaotambuliwa na Katibu Mkuu wataendelea kufanya shughuli za chama kama kawaida kwa mujibu wa katiba ya CUF.  
“Tamko la baraza hilo hatulitambui, haina maana yoyote ni mbwembwe, labda naweza nikasema hivi, kwanza baraza halali limekutana Machi 19, 2017 makao makuu ya chama mjini Unguja baada ya kamati ya utendaji taifa terehe Machi 2, 2017 kuandaa mkutano huo kwa mujibu wa katiba inavyoelekeza,” amesema na kuongeza.
“Katika mkutano wa baraza kuu, Wajumbe 43 walihudhuria kati ya 53 walio halali, kati yao 5 walikuwa na udhuru, hii inamaanisha wajumbe 48 wanamuunga mkono Katibu Mkuu, sasa hilo baraza la Lipumba lilikuwa na wajumbe wangapi? Lipumba si mwanachama keshafukuzwa, anaoufanya ni upuuzi mtupu hatuyatambui maamuzi yake na baraza lake.”
Kufuatia mgawanyiko huo, umepelekea kila upande kudai kuwa na bodi ya wadhamini ambapo upande wa Maalim jana ulisajiri bodi mpya ya wadhamini kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) hata hivyo Lipumba amedai kuwa RITA haiwezi kusajili bodi feki bila ya idhini yake kama Mwenyekiti wa Chama kwa kuwa aliiandikia barua.
Hali kadhalika kila upande unadai kuwa na baraza kuu la uongozi taifa, huku ikiteua mgombea wa ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, ambao ni Twaha Taslima upande wa Maalim Seif na mwengine ni miongoni mwa wale saba walioteuliwa na baraza la Lipumba.   
Na Regina Mkonde


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo