Wananchi wa kijiji cha Mengwe chini wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wanakabiliwa na tatizo la maji kwa miaka mitatu na wanalazimika kununua ndoo au debe moja kwa shs.1000/= kutoka kwa vijana wa boda boda walioligeuza tatizo hilo kuwa biashara yao.
Wakizungumza na mwandishi wa ITV ambayo ilishuhudia baadhi ya maeneo yakiwa na mabomba yameota kutu na koki za maji kuzingirwa na buibui wananchi hao wamesema, kilio chao ni cha muda mrefu lakini hakijapatiwa ufumbuzi.
Bi Anna Shayo amesema,yeye ni mteja wa maji wa kampuni ya maji ya Kilwater lakini bomba lake halijatoa maji tangu mwaka 2013 na wazazi kwa jumla wanaogopa kuwatuma watoto wao kwenda kutafuta maji umbali mrefu kwa hofu ya kubakwa njiani
Wakazi wengine wa kijiji hicho Bw Benardin Asenga na Evaline Shayo wameiomba serikali iwajengee mtandao mwingine wa maji katika kijiji hicho kutoka maeneo ya milimani ili kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo ambalo ni tofauti na vijiji jirani ambavyo vinapata maji
Meneja mkuu wa kampuni ya maji ya Kilwater Bw Prosper kessy amekiri kuwepo kwa tatizo hilo ingawa si kwa kijiji kizima ambalo limesababishwa na uharibifu wa miundombinu ya maji uliyofanywa na baadhi ya wananchi ambao utafanyiwa ukarabati.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Rombo Bi Agness Hokororo amesema,tatizo hilo ni kubwa kutokana na maji kidogo yanayozalishwa na Kilwater na serikali imeanza mchakato wa kuanzisha mamlaka ya maji ambayo itasimamiwa na Wizara ya maji ili kutosheleza mahitaji ya wananchi wa wilaya ya Rombo.