Wenyeviti wa Vijiji Matatani kwa Kupokea Rushwa ya Wafugaji

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, ameliagiza jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kilosa kuwachunguza wenyeviti wa serikali za vijiji, vitongoji na maofisa watendaji ili kubaini iwapo wamejilimbikizia mali zinazotokana na kupokea rushwa za wafugaji.
Alitoa agizo hilo kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Ulaya, Zombo na Kivungu wilayani humo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo ya wananchi na kubaini kuwepo kwa migogoro baina ya makundi hayo.
Kabla ya kutoa agizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi, alieleza mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji bado inaendelea katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Alisema migogoro ya aina hiyo kwa sasa ipo kwenye kata 14 za Kilangali, Ulaya, Masanze, Chanzuru, Rudewa, Msowero, Dumila, Kimamba, Magole, Mabwerebwere, Mikumi, Tindiga , Malolo na Zombo, zenye jumla ya vijiji 29.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa, aliitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kuwatumia Polisi na Takukuru kupita kila kijiji kuwachunguza wenyeviti wa vijiji, vitongoji na watendaji wao.
Alisema lengo la uchunguzi huo ni kuwabaini watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji na vitongoji wanatuhumiwa na wananchi kuchukua fedha za wafugaji na kuwaruhusu kuingia na mifugo yao katika vijiji bila kufuata utaratibu na idhini ya mikutano mikuu ya vijiji husika.
“Polisi na Takukuru anzeni na vijiji hivi 29 vilivyotajwa kuwa na migogoro ya mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji. “ Piteni kila kijiji muwachunguze Mwenyekiti wa kijiji, kitongoji na mtendaji wa kijiji ambao wametajwa na wananchi kwa tuhuma za kupokea fedha za wafugaji na kuwaruhusu waingie na mifugo yao na hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika,” alisisitiza Dk Kebwe.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mgoyi, alisema wilaya hiyo inaendelea na usajili na utambuzi wa mifugo ili kuwianisha idadi ya mifugo iliyopo na uwezo wa malisho.
Alisema hadi sasa wilaya imefanikiwa kusajili wafugaji 6,334 wenye jumla ya ng’ombe 176,031, mbuzi 122,948, kondoo 23, 436 na punda 2,258 katika maeneo mbalimbali wilayani humo, wakati ng’ombe wa asili wapatao 60,207 sawa na asilimia 34 wamepigwa chapa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo