Mtu wa kiume ambaye hajatambulika mara moja jina lake anayetuhumiwa kwa wizi wa mifugo ameuawa kwa kuchomwa moto mpaka kufa katika kijiji cha Ugabwa kata ya Lupalilo wilayani Makete usiku wa kuamkia leo
Kwa mujibu wa wananchi waliozungumza na mwandishi wetu eneo la tukio, wanasema limetokea leo usiku kati ya saa 7 na saa 8, ambapo watuhumiwa hao walikuwa wawili wakiwa na mbuzi wawili waliokuwa wamewabeba kwenye tenga wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki, ndipo watu ambao hawafahamiki walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja na kumuua kwa kumchoma moto yeye pamoja na pikipiki inayodaiwa kutumika katika tukio la wizi wa mbuzi hao
Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Nyamo Sanga ambaye amesema mbuzi hao ni wa kwake, akizungumzia tukio hilo amesema aliamshwa na mwenyekiti wa kijiji usiku majira ya saa 8 na walipofika eneo la tukio walikuta moto ukiwaka na kuogopa kusogelea eneo hilo mpaka ulipozimika na ilipofika alfajiri aliweza kuwagundua mbuzi waliokuwa wamefungwa pembezoni mwa mwili wa marehemu wanaodaiwa kuwa wameibiwa kuwa ni wa kwake
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Bi Anahuruma Amulike amesema taarifa za kutokea kwa tukio hilo amezipata asubuhi baada ya kuamshwa na jirani yake huku akisisitiza kwamba tukio hilo ni baya na haungi mkono kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi, na wale wenye tabia kama hizo waache na wajishughulishe na shughuli halali za kuwapatia kipato
Mzee Daudi Vilumba ambaye nyumba yake iko mita chache kutoka lilipotokea tukio hilo amesema alilisikia kelele wakati likitokea na kutokana na uzee wake walifanya jitihada za kuujulisha uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na mkewe
Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Obadia Sanga akizungumza na mwandishi wetu eneo la tukio amesema tukio hilo ni mara ya kwanza kutokea katika kijiji chake na ameelezea mazingira ya kutokea kwake
Nikolaus Andrea Sanga ni Afisa mtendaji wa kijiji hicho ambapo ameelezea hatua alizozichukua yeye kama kiongozi wa serikali kijijini hapo mara baada ya tukio hilo ikiwemo kutoa taarifa kwa jeshi la polisi
Akithibitisha kifo cha marehemu huyo Daktari Tabibu kutoka hospitali ya wilaya ya Makete Traiphon Mayala ameelezea sababu za kifo cha marehemu baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wake kuwa alipigwa na vitu mbalimbali mwilini mwake vilivyosababisha majeraha na kuvuja damu nyingi na kufariki dunia ndipo akachomwa moto
Jeshi la polisi Makete limefika eneo la tukio na kuchukua taarifa za mauaji hayo na kuruhusu mwili huo ambao umeungua kiasi cha kutotambulika uzikwe
sikiliza sauti zote za tukio hilo kwa kubonyeza play hapo chini