Watuhumiwa 13 wa mauaji ya watumishi watatu kutoka katika chuo cha utafiti wa udongo na maendeleo ya ardhi kutoka katika chuo cha Seliani Mkoani Arusha wamefikishwa mahakamani kwa mara ya pili ambapo hati yao ya mashtaka imebadilishwa.
Gari waliyokuwa wakitumia watafiti hao baada ya kuchomwa moto
Watuhumiwa hao kila mmoja alisomewa shitaka la mauaji ya watafiti hao watatu ambao ni Nicas Magazine aliyekuwa dereva, Theresia Nguma na Faraji Mafuru waliokuwa watafiti katika kijiji cha Iringa Mvumi kilichopo katika Wilaya ya Chamwino kwa kuwadhania kuwa ni wanyonya damu.
Awali Oktoba 17 mwaka huu washtakiwa hao kwa pamoja walishtakiwa kwa kosa la kuwauwa watumishi hao watatu lakini jana hati yao ya mashtaka ilibadilishwa ambapo kila mmoja alisomewa shtaka la kuwauwa watumishi hao.
Akisoma mashtaka yao mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Dodoma Joseph Fovo, Wakili wa serikali Beatrice Nsana alisema kuwa kila mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kumuua Nicas Magazine, Theresia Nguma na Faraji Mafuru kinyume na kifungu cha sheria cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu.
Baadhi ya watuhumiwa walipokuwa wakipelekwa mahakani kwa mara ya kwanza
hata hivyo hakimu Fovo aliwataka washtakiwa hao kutokujibu kitu chochote kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji ambapo kesi hiyo itatajwa tena hadi Novemba 14 mwaka huu ambapo watuhumiwa wote wamerudishwa rumande.
Wanaoshtakiwa katika kesi hiyo ni wanawake wanne na wanaume tisa ambao ni wakazi wa kijiji cha Iringa Mvumi katika wilaya ya Chamwino yalipotokea mauaji hayo.
Watuhumiwa hao ni Cesilia Mwalu, Dorca Mbehu, Edna Nuno, Grace Masaulwa, Juma Madeha, Alberth Chimanga, Sosteness Mseche, Julius Chimanga, David Chimanga, Lazaro Kwanga, Yoram Samamba, Edward Lungwa na Simon Samamba