Serikali imemfuta cheo mratibu wa mfuko wa maendeleo ya jamii-TASAF- wilaya ya Kinondoni Bwana Onesmo Koyamba na kulitaka jeshi la Polisi kushirikiakiana na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa- TAKUKURU kuchunguza tuhuma zinazomkabili ikiwemo upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 266 zinazodaiwa kupewa wananchi masikini hewa.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Kinondoni Bwana Ali Hapi wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema mbali na tafiti kuonyesha kaya masikini hewa 537 kulipwa kiasi hicho cha fedha, uchunguzi umebaini majina ya watumishi wa serikali na wafanyabiashara zaidi ya 517 wameshalipwa zaidi ya shilingi milioni 180.3 na kusisitiza tayari uamuzi umeshafanyika wa kuondoa orodha ya majina hao katika kunufaika na fedha hizo na kuwafikisha katika mikono ya sheria.
Aidha Bwana Hapi ameshauri mamlaka husika kuangaliwa upya mfumo na upatikanaji wa wananchi walengwa wanaotakiwa kunufaika na fedha hizo, taratibu za ulipaji wa fedha na mfumo wa usimamizi ili kudhibiti upotevu wa fedha,huku mtendaji kata ya Kinondoni Bwana Amiri Bakari ametaka kuwepo kwa utaratibu rasmi wa wazi utakaoanzia katika ngazi ya chini ya serikali ya mtaa ili kuhakiki hali ya umasikini kwa walengwa pamoja na idadi.