Mkuu wa wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri amelifunga darasa moja la shule ya msingi Iditima katika kijiji cha Itambo tarafa ya Lupembe baada ya kukagua shule hiyo na kubaini kuwa darasa hilo la wanafunzi wa darasa la sita linahatarisha usalama wa wanafunzi kwa kubomoka ukuta wa upande mmoja.
Aidha ameuagiza uongozi wa kata hiyo na kijiji kwa kushirikiana na Afisa tarafa wa tarafa hiyo ya Lupembe kulirekebisha jengo hilo kwa kupanua vyumba vya madarasa mawili kwa kua vimekuwa vidogo kufuatia ujenzi wa mfumo wa kale.
Shule hiyo ya iditima inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo uchakavu wa sakafu, na bendera ya taifa ubovu wa madawati ,pamoja na uhaba wa samani kama meza za walimu na viti jambo ambalo linatia mashaka upatikanaji wa taaluma bora shuleni hapo
Kaimu mkuu wa shule hiyo ya Iditima Wilfred Chembela amesema kuwa kwa sasa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vine vya madarasa na kwamba wazazi kijijini hapo wanaendelea na maandalizi ya tofali na mawe kukabiliana na changamoto hiyo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Bi Monica Kwiluhya amemuhakikishia mkuu wa wilaya kutoa ushirikiano katika kuondoa kero zinazoikabili shule hiyo ikiwa ni pamoja na kukarabati madarasa ya ambayo hayana saruji na kuchangia sehemu ya ujenzi wa madarasa hayo.
Na Prosper Mfugale