Kifo cha Thomas Mashali, Serikali yamlilia


Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa pamoja na Chama cha Wanandondi nchini kufuatia kifo cha Bondia wa ngumi za kulipwa Bw. Christopher Fabian Mashale maarufu kama ‘Thomas Mashali’ kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 31/10/2016. 

Mhe. Nape Nnauye pamoja na watendaji wa Wizara wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha bondia huyo na kuongeza kuwa kifo hicho ni pigo katika tasnia ya michezo nchini. 

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha bondia Thomas Mashali, sina maneno ya kuelezea masikitiko na huzuni niliyonayo, kwani kifo chake ni pigo katika tasnia ya masumbwi nchini” alisema Mhe.Nnauye. 

Aidha, Waziri Nape Nnauye ameitaka jamii na wanamichezo kote nchini kuwa wavumilivu na watulivu wakati wote wa msiba na kumuombea marehemu makao mema kwa Mwenyezi Mungu. 

Thomas Mashali alizaliwa Jijini Dar es Salaam tarehe 9 Septemba, 1989 na kuweza kushiriki katika baadhi ya michezo mbalimbali ya masumbwi ya kulipwa ambapo kati ya michezo 26 aliyowahi kucheza alishinda michezo 19, ambayo tisa ni ya Knock Out (KO), lakini pia alipoteza michezo mitano yaani KO minne na kutoka sare mchezo mmoja. 

Bondia Thomas Mashali aliwahi kupigana na baadhi ya mabondia maarufu wa ndani na nje ya nchi wakiwemo Francis Cheka, Abdallah Paziwapazi, Ibrahim Tamba na wengineo. 

Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amina. 
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini 
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo 

31 Oktoba, 2016 .


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo