Akizungumza na mtandao huu, nyumbani kwake Tandale kwa Mtogole jijini Dar, mzee Mashali alisema taarifa za kifo cha mwanaye alizipata leo alfajiri kupitia kwa vijana watatu ambao walifika nyumbani hapo pasipo kujitambulisha majina yao na kumfikishia taarifa kuwa Mashali kafikikishwa katika Hospitali ya Sinza (Palestina) akiwa hajitambui kutokana na kipigo alichopigwa na watu wasiojulikana.
“Baada ya taarifa hizo niliwasiliana na ndugu zake wengine akiwemo dada yake ambao walikwenda Palestina kufuatilia lakini walimkuta ameshapewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili ingawa tayari pale walishaelezwa alikuwa ameshafariki dunia kutokana na kupigwa sana kichwani.
“Kuhusu suala la mazishi bado hatujajua lini tutazika kwa sababu maiti imehifadhiwa Muhimbili, halafu kuna mambo ya uchunguzi wa kipolisi yanatakiwa yafanyike na baadaye ndiyo tutajua lini tutazika. Nimeumizwa na kifo chake kwa sababu mara ya mwisho niliongea naye jana katika simu,” alisema baba Mashali.
Naye dada wa marehemu, Josephine Mashali alisema amepokea taarifa za kifo cha kaka yake kwa masikitiko makubwa na anamuomba Mungu ampumzishe kwa amani katika nyumba yake ya milele.
Marehemu Mashali ameacha jumla ya watoto watano wote wakiwa ni wa kike.
Na Denis Mtima/Gpl