
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma Lazaro Mambosasa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu sita kwa makosa mbalimbali yanayohusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Dodoma, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma Lazaro Mambosasa amesema vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni kosa kisheria, lakini watu wamekuwa wakivinyamazia vitendo hivyo kwa kuwa vinahusisha watu wa karibu baina ya watendewa na wahalifu.
Uhalifu huo unawaathiri zaidi watoto wadogo ambapo yapo matukio ya kujeruhi watoto, kuua na kutupa watoto ambapo Kamanda Mambosasa ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Dodoma kutokaa kimya dhidi ya wahalifu wa aina hiyo
Kamanda Mambosasa amewataka wananchi watoe taarifa katika vituo vya polisi na watumie vema madawati ya jinsia na watoto yaliyopo katika vituo vya polisi vya wilaya zote za Dodoma.
Watuhumiwa waliokamatwa watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapo kamilika.