Warundika takataka ofisini kwa Mwenyekiti wa Mtaa

WAKAZI wa Mtaa wa Mwembeni, kata ya Manzese jijini Dar es Salaam wamelazimika kuzikusanya taka na kuzipeleka kwenye Ofisi ya Mwenyekiti wa mtaa huo kwa madai ya gari la taka kutopita kuzoa taka hizo kwa kipindi cha miezi mitatu.

Wamedai uamuzi huo ni funzo kwa uongozi huo ili wawajibike ipasavyo hasa kwa kuzingatia kuwa wamekuwa wakilipa fedha kwa ajili ya kuzoa taka. Wakizungumza katika ofisi hiyo wamedai kuwa kila kaya imekuwa ikitozwa Sh 2,000 kwa ajili ya uzoaji taka lakini kwa kipindi cha miezi mitatu taka hizo hazijazolewa.

Akizungumza kwa niaba ya Mjumbe wa eneo hilo, Majaliwa Kassim alisema, viongozi wa mtaa huo wamekuwa wakiwahamasisha kulipa ada ya uzoaji taka lakini wanashangazwa kuwa taka hizo hazizolewi.

Aidha, alisema, wataendelea kukusanya taka hizo na kuzipeleka kwenye ofisi hiyo hadi pale Mwenyekiti huyo pamoja na viongozi wenzake watakapojirekebisha.

Hata hivyo Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Fatuma Abdallah alisema, wakazi hao wamekuwa wakigoma kuchangia fedha kwa ajili ya uzoaji wa taka hizo jambo linalomfanya ashindwe kuagiza gari kutoka Manispaa kwa ajili ya kuzipeleka dampo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo