Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN
amewahakikishia watanzania kuwa serikali ya awamu ya TANO inadhamira ya
dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii kwa
kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi,kudhibiti matumizi
yasiyolazima, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa kodi ili fedha
zinazokusanywa zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.
Makamu
wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN amesema hayo kwenye kilele cha maadhimisho
ya sikukuu ya NANE NANE kitaifa katika uwanja wa NGONGO Manispaa ya
LINDI mkoani LINDI kwa naiba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dakta JOHN POMBE MAGUFULI.
Katika
hutoba yake kwa mamia ya wananchi waliofurika katika viwanja vya
NGONGO, Makamu wa Rais amesema azma ya serikali ya kuwaletea wananchi
maendeleo itatimia iwapo tu wananchi wataunga mkono jitihada za serikali
katika kulipa kodi kwa wakati,kudai risiti,kufanya kazi kwa bidii,
kukemea vitendo vya rushwa kama hatua ya kufikia uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2020.
“Napenda
kuwahakikishia kuwa tuna dhamira ya dhati ya kuendelea kuwatumikia na
kuwaboreshea huduma zote za kijamii pamoja na kukuza uchumi wa nchi kwa
ujumla bila kujali mikoa mnayotoka,jinsia,dini au itikadi za vyama
vyenu.”
Kuhusu
uimarishaji wa shughuli za kilimo nchini, Makamu wa Rais SAMIA SULUHU
HASSAN amesema maadhimisho ya sikukuu ya NANE NANE ni moja katika ya
juhudi za serikali za kuboresha shughuli za kiuchumi katika taifa ambapo
asilimia 75 ya wananchi wanajihusisha na shughuli za kilimo,mifugo na
uvuvi kote nchini.
Amesisitiza
kuwa serikali itaendelea kuzipa kipaumbele sekta za kilimo,mifugo na
uvuvi na kuongeza bajeti katika sekta hizo ili ziweze kuchangia kwa
kiasi kikubwa katika kuongeza pato la taifa na uchumi wa nchi kwa
ujumla.
Makamu
wa Rais ameeleza wananchi kuwa serikali imeweka mikakati na mipango
inayolenga kusaidia uimarishaji wa shughuli za kilimo kote nchini kwa
kuongeza matrekta makubwa na madogo kutoka 7,491 mwaka 2005/2006 hadi
16,478 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hivyo kupunguza matumizi ya jembe la
mkono kutoka asilimia 70 hadi asilimia 12.
Aidha
amefafanua kuwa serikali imeongeza idadi ya maafisa ugani katika kilimo
kutoka 3,379 mwaka 2005 hadi 2006 hadi 8,756 mwaka 2015/2016 na
serikali pia imefufua mashamba ya mbegu kwa kuhusisha sekta binafsi,
Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa katika kuzalisha mbegu bora
za mazao ya chakula nchini.
Kwa
Upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dakta PHILIP MPANGO amehimiza
wananchi kote nchini kulipa kodi ipasavyo ili fedha zitakazopatikana
zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara kwa
kiwango cha lami huku Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles
Mwijage akiwataka wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara waongeze
uzalishaji wa mazao ya biashara ambayo watauza ndani na nje ya nchi
katika hatua ya kukuza pato la familia na taifa kwa ujumla.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
8-Aug-16
