Akizungumza
wakati wa kuaga miili ya askari watatu kati ya wanne wa Jeshi la Polisi
waliouawa wiki hii katika tawi la benki ya CRDB lililopo Mbande
wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Makonda alisema jambazi
atakapokutwa popote iwe msituni iwe wapi agongwe na apigwe.
Alisema
alipopata taarifa ya vifo vya askari hao wanne alifungua pazia za
madirisha nyumbani kwake na kuwaangalia askari wanaolinda na kulia kwa
uchungu na kwamba usiendelezwe ukichaa wa haki za binadamu kwani ni
uendawazimu ambao hauwezi kuvumilika.
“Kamanda
Sirro (Simon) mimi ndiyo mkuu wako wa mkoa nasema ukikamata hao watu
popote gonga, piga na watu wa haki za binadamu wakija waambie waje
kwangu, hatuwezi kukaa kwenye mkoa ambao haupo salama,” alisema
Makonda aliyedai hana maneno mazuri ya kusema kwa sababu hakuumbwa
kumfurahisha mtu, bali anafanya kazi ya Mungu na wakati wake ukiisha
ataondoka.
“Kama
kuna haki za binadamu nataka haki za askari wangu kwanza. Kama hao watu
wa haki za binadamu wapo nataka kuona wakiandamana kukilaani kitendo
hiki, ”alisema Makonda.
Hata
hivyo, kauli hiyo ya Makonda imepingwa na wanasheria wakidai kuwa
mwenye haki ya kutoa hukumu ya kuadhibiwa au kutoadhibiwa ni mahakama na
si mtu mwingine.
Wakili
kutoka Crax Law Partners, Hamza Jabir alisema kisheria mtu yeyote
anapokamatwa kwa tuhuma yoyote anakuwa ni mtuhumiwa hivyo hakuna mwenye
haki ya kumhukumu.
Alisema
baada ya kufanyika uchunguzi wa kubaini tuhuma hizo kama za kweli au
la, anapelekwa mahakamani na mahakama ndiyo pekee yenye haki ya kuhukumu
kama kwa kosa alilokutwa nalo ana haki ya kufungwa, kupigwa au kuuawa.
“Kutoa hukumu bila kufuata taratibu za kisheria ni kuingilia uhuru wa mhimili wa sheria ambao unajitegemea, ”alisema Jabir.
Wakili
wa kujitegemea Juma Nassor alisema anayetuhumiwa kwa kosa lolote
ikiwamo kuua, adhabu yoyote anayopaswa kupewa, mwenye haki ya
kuidhinisha na kuitamka adhabu hiyo ni mahakama.
