Mrema Ataka TLP na CCM Viungane Kuanzisha UKAWA Mpya

Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema amesema pamoja na Rais John Magufuli kufanya kazi vizuri, hawezi kurejea CCM na badala yake amependekeza vyama hivyo viwili viunde ushirikiano wao kama ilivyo kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani, pia amesema kuna haja ya suala la maandamano na mikutano ya kisiasa kuundiwa kanuni ili kuondoa malalamiko ya vyama vya upinzani kuzuiwa kutekeleza haki hiyo ya kikatiba.

Mrema, ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM.

Alikuwa ameulizwa na mmoja wa wasikilizaji wa kipindi hicho kwa nini asirejee CCM kama anaridhika kuwa Rais Magufuli anatekeleza yale ambayo alitaka yafanyike lakini hayakufanyika hadi akaamua kuisaliti Serikali ya Awamu ya Pili na kuihama CCM na kwenda NCCR-Mageuzi kabla ya kuanzisha chama cha TLP.

Mrema alijibu swali hilo kwa kuanza kueleza historia yake na mambo aliyofanya wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika kupambana na uhalifu na kwamba alipoona anatofautiana na Serikali aliamua kujitoa.

Alisema CCM chini ya Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli inafanya vizuri kwa kutekeleza yale aliyokuwa akiyataka wakati akiwa waziri.

Alisema Rais Magufuli anatoa ushirikiano kwa kila mtu, hivyo atakuwa bega kwa bega kumsaidia kiongozi huyo aliyedai anatekeleza majukumu yake kwa uwazi.

“Hiyo Ukawa nyingine siipendi kwa sababu haijui inataka kufanya nini.”

Mrema, ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya TLP mwaka 2010 hadi 2015, alisema ataendelea kumwamini Rais Magufuli kutokana utendaji kazi wake kazi mzuri, ikiwamo kupambana na ufisadi, kazi ambayo alisema anapenda aone ikifanyika.

Akizungumzia uamuzi wa Rais Magufuli kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa, Mrema alisema agizo hilo ni sahihi kwa sababu hakuna haja ya mikutano wakati uchaguzi ulishapita.

Lakini alipoulizwa kama Serikali ingezuia mikutano na maandamano wakati alipoihama CCM mwaka 1995, Mrema, ambaye alivuta hisia za wengi wakati huo alisema katika kipindi hicho Rais hakuwa Magufuli.

Alisema kama Magufuli angekuwa ni Rais wakati huo na anatekeleza hayo aliyokuwa anataka, angekubaliana na uamuzi wa kuzuia maandamano.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo