Wananchi wa Mtaa wa Mtawala Kata
ya Mji Mpya Manispaa ya Morogoro mkoani hapa, wamelizingira gari la
matangazo ya kujiunga na jamii ya Freemason wakitaka kulichoma moto
kufuatia dereva wake kumgonga Janeth Ngolika muuza mbogamboga mitaani.
Tukio hilo lilijiri wiki iliyopita maeneo hayo ya Mtawala ambapo mashuhuda, Asha Juma na John Lazaro walikuwa na haya ya kusema:
“Huyu mwanamke alikuwa na kapu lake la
mboga, wakati anakatiza barabara ghafla lilitokea gari la matangazo ya
Freemason likiwa mwendokasi na kumgonga kisha nalo likatumbukia
mtaroni,” alisema John.
Kwa upande wake Asha alisimulia:
“Nimeshuhudia hili gari (Toyota Noah) la matangazo ya Freemason
likimgonga na watu kutaka kulichoma moto kwa sababu yule mama aliumia
sana na alikuwa akitokwa damu usoni.”
Mwandishi wetu alilishuhudia gari hilo
likiwa na ‘chata’ za Freemason likiwa mtaroni hapo kwa muda mrefu huku
dereva wake akitokomea kusikojulikana.
Baada ya kuondoka eneo la tukio,
mwanahabari wetu alitinga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na
kumkuta Janeth akiwa hoi kitandani.
Akizungumza na Wikienda kwa
tabu, mwanamke huyo alieleza mkasa huo: “Nilikuwa kwenye biashara yangu
ya kuuza mboga. Nilipofika maeneo ya Mtawala niligongwa na gari na
kupoteza fahamu hadi nilipozinduka nikiwa hapa (hospitalini).”
Kwa takriban mwezi mzima sasa, gari hilo
limekuwa likizunguka mitaani mjini hapa likiwahamasisha wananchi
kujiunga na kundi hilo.
chanzo:GPL
